Vita tu ndio wafahamucho watoto 3 kati ya 4 waliozaliwa Sudan Kusini -UNICEF

8 Julai 2018

Watoto milioni 2.6 nchini Sudan Kusini wamezaliwa wakati wa vita vilivyoibuka mwaka 2013, ikiwa ni miaka miwili tu tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mwaka 2011.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema idadi hiyo ni kati ya watoto milioni 3.4 waliozaliwa tangu nchi hiyo ipate uhuru.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini New York, Marekani na Juba Sudan Kusini, ambayo ni mkesha wa maadhimisho ya miaka 7 ya uhuru wa nchi hiyo imesema watoto hao wamefahamu vita tu na kwamba migogoro isiyoisha imedumaza maendeleo ya Sudan Kusini.

Imesema watoto wameachwa wakiwa na utapiamlo na kushambuliwa na magonjwa mengi, pamoja na unyanyasaji ikisema mategemeo ya mustakabali mwema kufuatia uhuru wa mwaka wa 2011 yalitoweka muda mfupi baada ya kulipuka tena mapigano ya wenyewe kwa wenyewe  mwezi disemba mwaka 2013.

UNICEF/Bullen Chol
Mei 17,2018 Pibor Sudan Kusini watoto 210 waiachiliwa kirasmi na makundi yenye silaha.Msaada wa kiutibabu na wa kisayikolojia unatolewa na UNICEF na washirika wake.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta H. Fore, ambaye  alitembelea miji ya Juba, Ganiyel na Bentui, Sudan Kusini mapema mwaka huu, amesema kuwa wakati Sudan Kusini, ikifikisha miaka saba tangu ijinyakulie uhuru wake,vita visivyoisha vinaendelea kuvuruga maisha ya watoto milioni kadhaa. Makundi yanayohasimiana yanaweza na ni lazima yafanye juu chini kurejesha amani . watoto wa Sudan Kusini wanahitaji maisha bora.”

Amesema ingawa watoto 800 wameachiliwa huru  kutoka makundi yenye silaha tangu mwanzo wa mwaka huu , lakini takriban watoto wengine 19,000 wanaendelea kutumikishwa kama wapiganaji,wamegeuzwa wapishi, wabeba mizigo, na wajumbe .

Kama hiyo haitoshi, Bi. Fore amesema wengine wanaendelea kukabiliana na mateso  na ukatili wa   kingono ambao idadi yao imepanda kutoka 500 wakati vurugu zilipoanza mwaka wa 2013.

UNICEF inasema kiwango cha wasiojua mlo utatoka wapi kimepanda kutoka asilimia 35 mwaka 2014 hadi karibu asilimia 60 kufikia sasa na sehemu kadhaa za taifa hilo zinakabiliwa na njaa hasa wakati wa msimu wa mavuno machache.

Viongozi wa kisiasa waheshimu makubaliano

Halikadhalika utapiamlo umefikia viwango vya juu na karibu watoto zaidi ya milioni moja wana utapiamlo  na  wengine 300,000 wako vibaya sana wanakaribia kufa.

Bi. Fore amesema kuwa kutia sahihi makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano kati ya makundi mawili makuu mjini Khartoum nchini Sudan mwezi jana ni hatua moja mbele katika juhudi za kuleta amani ambazo zimekuwa zikigonga mwamba kila mara.

Ameongeza kuwa, “ sasa ni wajibu wa viongozi pamoja na makamanda kuheshimu makubaliano hayo huku ikitarajiwa kuwa  wafanyakazi za utoaji misaada  wataruhusiwa kwenda mahali popote bila kizuizi kufanya kazi zao.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud