Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waandamanaji wanapaswa kujilinda, na kuwalinda wengine dhidi ya COVID-19-WHO

Waandamanaji Brooklyn, New York Marekani wakiandamana kwa amani kuhusu ukosefu wa haki na ubaguzi wa rangi
UN News/ Shirin Yaseen
Waandamanaji Brooklyn, New York Marekani wakiandamana kwa amani kuhusu ukosefu wa haki na ubaguzi wa rangi

Waandamanaji wanapaswa kujilinda, na kuwalinda wengine dhidi ya COVID-19-WHO

Afya

Waandamanaji ambao wanataka kwenda mitaani ili kupaza sauti zao ambazo wanataka zisikike, wanatakiwa kuchukua kila tahadhari ya kutokuambukizwa virusi vya corona au kuwaambukiza wengine, katika kipindi hiki ambacho bado mlipuko huu haujakaribia mwisho wake, limesema shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO.

Ujumbe huo wa WHO uliotolewa na msemaji wake mjini Geneva Uswisi, unakuja wakati ambapo nchini Marekani kuna maandamano yanayoendelea kupinga kuuawa wa George Floyd, na pia katika kipindi ambacho linategemewa wimbi la pili la maambukizi katika nchi ambako sheria za kusalia ndani zimeanza kulegezwa. 

“Mapambano hayajaisha hadi pale ambapo hakutakuwa na virusi popote duniani. Kwa hivyo mambo yote ambayo tumekuwa tukiyasema, bado yanafanya kazi. Tahadhari nzuri ni kumudu kukaa mita moja kati ya mtu na mtu, kuweza kunawa mikono, kuhakikisha kuwa hugusi midomo yako, pua na macho. Tumeona watu ambao wameona ni muhimu kutoka nje kupaza sauti zao lakini tunawasihi kukumbuka: endelea kujilinda na kuwalinda wengine, corona ipo, jilinde na uwalinde wengine wakati unaeleza kuhusu hisia zako.” Ameeleza msemaji wa WHO Dkt Marget Harris. 

Mambukizi katika Marekani yanasikitisha

Kupitia mkutano na vyombo vya habari kwa njia ya televisheni, Dkt Harris ameeleza kuwa viwango vya maambukizi miongoni mwa Wamarekani ambayo kwa sasa ni kitovu cha maaambukizi, “ni ya kusikitisha, kutisikitisha sana.”

Kwa mujibu wa takwimu za sasa za WHO, Marekani ina vifo 106,000 kutokana na COVID-19 na zaidi ya watu milioni 1.8 wamethibitishwa kuwa na maambukizi.