COVID-19 ni msumari wa tatu kwa wakimbizi na wahamiaji- Guterres

Uthibitisho wa kitambulisho Kambi ya wakimbizi ya Kakuma
WFP/Florence Lanyero
Uthibitisho wa kitambulisho Kambi ya wakimbizi ya Kakuma

COVID-19 ni msumari wa tatu kwa wakimbizi na wahamiaji- Guterres

Wahamiaji na Wakimbizi

Janga la virusi vya Corona, COVID-19  likiendelea kuzua kizaazaa maeneo mbalimbali duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa tamko lake likitaka hatua zaidi kusaidia wakimbizi, wakimbizi wa ndani na wahamiaji ambao amesema kwa makundi hayo janga hilo ni sawa na mwiba wa tatu katika majanga ambayo wanakumbana nayo.

Guterres amesema kuwa, watu hao wamelazimika kukimbia makwao kutokana na sababu lukuki ikiwemo majanga ya asili, vita na hata mazingira magumu.

COVID-19 ni janga juu ya majanga wakimbizi na wahamiaji

“Hivi sasa watu hao wanakumbwa na majanga matatu kwa wakati mmoja, mosi, janga la kiafya, kwani wanapoambukizwa virusi, mara nyingi kwenye maeneo walimojazwa kupindukia na ambako kutochangamana hakuwezekani, huduma ya afya, maji na huduma za kujisafi, lishe ni sawa na anasa. Na hali ni mbaya zaidi kwa nchi zinazoendelea na zaidi ya yote theluthi moja ya wakimbizi wa ndani wamo kwenye mataifa yaliyo hatarini zaidi kupata COVID-19.”

Katibu Mkuu ametaja janga la pili kuwa ni watu hao wanakumbwa na janga la kiuchumi na kijamii, hasa wale wanaofanya kazi kwenye sekta isiyo rasmi bila kuwa na fursa ya kunufaika na mfumo wa hifadhi ya jamii.

 “Ukosefu wa kipato kutokana na COVID-19, kunaweza kusababisha anguko la utumaji wa fedha kwa thamani ya dola bilioni 109, hii in sawa na robo tatu ya misaada rasmi ya maendeleo, ikimaanisha watu milioni 800 wanaotegemea fedha hizo huko nyumbani hawatozipata,” amesema Katibu Mkuu.

Mtoto wa kike kutoka Niger ambaye ana ujauzito wa mapacha baada ya kutumikishwa kwenye ukahaba baada ya kuwasili nchini Italia kupitia bahari ya Mediteranea akitoka Libya. Hapa ni kwenye makazi ya hifadhi huko Asti, mkoa wa Piedmont Italia. (2017)
© UNICEF/Alessio Romenzi
Mtoto wa kike kutoka Niger ambaye ana ujauzito wa mapacha baada ya kutumikishwa kwenye ukahaba baada ya kuwasili nchini Italia kupitia bahari ya Mediteranea akitoka Libya. Hapa ni kwenye makazi ya hifadhi huko Asti, mkoa wa Piedmont Italia. (2017)

Janga la tatu ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu ni kwamba watu hao hawana ulinzi akisema kuwa, “zaidi ya nchi 150 zimeweka vizuizi mipakani ili kuepusha kusambaa kwa virusi vya Corona. Takribani nchi 99 zimekuwa na kanuni malum kwa watu wanaosaka hifadhi au wanaokimbia mateso. Na wakati huo huo, COVID-19 imechochoea chuki dhidi ya wageni, ubaguzi wa rangi na unyanyapaa.”

 Ameongeza kuwa, wanawake na wasichana ambao tayari hali yao si nzuri, wanazidi kuwa katika hatari zaidi, amesema Bwana Guterres akitaja ukatili wa kijinsia na unyanyaswaji.

Pamoja na kwamba wakimbizi na wahamiaji wanakumbwa na changamoto hizo, Katibu Mkuu amesema kuwa bado wanajitolea kishujaa kuwa mstari wa mbele kufanya kazi muhimu akitoa mfano kuwa, “takribani muuguzi mmoja kati ya wanane duniani kote anafanya kazi katika nchi ambayo si taifa lake la kuzaliwa.”

 

Misingi minne ya kuzingatia kunusuru wahamiaji na wakimbizi

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu anataka katika janga hili la Corona kufirikia upya mienendo au hamahama ya kibinadamu kwa kuzingatia misingi mikuu minne.

Misingi hiyo ni mosi, kutambua kuwa kuengua mtu ni gharama kubwa kuliko kumjumuisha akisema kuwa, “mfumo jumuishi wa afya, kijamii na kiuchumi utasaidia kukabili virusi na kuanzisha upya uchumi na kusongesha malengo ya maendeleo endelevu. Pili lazima tuzingatie utu tunapokabiliana na janga hili na tujifunze kutoka katika nchi chache ambazo zimeonesha jinsi ya kudhibiti mipaka huku zikiheshimu haki za binadamu, na kanuni za kimataifa za kulinda wakimbizi.”

Wakimbizi na wahamiaji wakiwa katika mpaka wa Pazarkule eneo la mpakani mwa Uturuki wakiwa na matumaini ya kuvuka na kuingia Ugiriki.
© UNICEF
Wakimbizi na wahamiaji wakiwa katika mpaka wa Pazarkule eneo la mpakani mwa Uturuki wakiwa na matumaini ya kuvuka na kuingia Ugiriki.

Msingi wa tatu ni kutambua kuwa hakuna mtu aliye salama hadi pale kila mtu yuko salama hivyo uchunguzi, tiba na chanjo lazima ziwafikie watu wote na nne ni kuhakikisha kuwa wakimbizi na wahamiaji ni sehemu ya suluhisho. “Hebu na tuondoe vikwazo visivyo na maana, tusake mbinu mpya za kuhalalisha njia kwa wahamiaji na kupunguza gharama za utumaji wa fedha,”  amesema Katibu Mkuu.

 Katibu Mkuu amerejelea kauli yake kuwa hakuna taifa ambalo linaweza kukabili janga la Corona peke yake au hata suala la uhamiaji.

 “Lakini kwa pamoja, tunaweza kudhibiti kusambaa kwa virusi, tukahimili athari zake hasa kwa wale walio hatarini zaidi na tukaibuka bora kwa maslahi ya wote,” ametamatisha Katibu Mkuu.