COVID-19 yaongeza chumvi katika kidonda cha LGBTI

17 Mei 2020

Hii leo dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, waliobadili jinsia na wale wenye wapenzi wa jinsia zote, IDAHOT, katika changamoto kubwa, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii ya leo 17 Mei.

Guterres amesema, “miongoni mwa athari kubwa za ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19, ni ongezeko la kuweko hatarini kwa watu wa kundi hilo au LGBTI. Tayari wakikabiliwa na ubaguzi, mashambulizi na kuuawa, kwa sababu tu ya wao ni nani na nani wameamua kumpenda, watu hao wanakabiliwa na unyanyapaa mkubwa kutokana na virusi vya Corona na pia kutokana na vikwazo wanavyopata wakati wakisaka huduma za afya.”

Katibu Mkuu amesema kuna ripoti ya kwamba maelekezo kuhusu COVID-19 yanatumiwa vibaya na polisi ili kulenga wapenzi wa jinsia moja au waliobadili jinsia na mashirika yao.

“Kadri janga hili linavyozidi kuibuka, Umoja wa Mataifa utaendelea kuangazia vitendo hivyo na vinginevyo pamoja na umuhimu wa kila mtu kulindwa na kujumuishwa katika hatua dhidi ya janga la Corona,”  amesema Katibu Mkuu.

Ametamatisha ujumbe wake akisema kuwa “kwa pamoja hebu na tuungane dhidi ya ubaguzi na kwa haki ya kila mtu kuishi huru na usawa katika utu na haki.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter