Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atuma salamu za pole kwa waathirika wa ajali ya ndege na Kimbunga

Mafuriko nchini Pakstan
UN Photo/WFP/Amjad Jamal
Mafuriko nchini Pakstan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atuma salamu za pole kwa waathirika wa ajali ya ndege na Kimbunga

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, hii leo kupitia msemaji wake, amesema amesikitishwa na kupotea kwa maisha na kujeruhiwa kwa abiria wa ndege ya abiria iliyoanguka mjini Karachi Pakistani jana Ijumaa. 

“Katibu Mkuu anatuma salamu zake za rambirambi kwa familia za waathirika na pia kwa watu na serikali wa Pakistan. Anawatakia ambao wamejeruhiwa, kupona haraka.” Umesema ujumbe wa Katibu Mkuu. 

Duru za vyombo mbalimbali vya kimtaifa zinaeleza kuwa ndege hiyo ya abiria iliyokuwa imebeba watu zaidi ya 99 ikitokea Lahore kwenda Karachi ilianguka katika maeneo yenye msongamano wa watu mjini Karachi ilipojaribu kutua mara mbili bila mafanikio. Taarifa zinaeleza kuwa ni watu wawili pekee walionusurika. 

Katika ujumbe mwingine, Bwana Guterres, amesema amesikitishwa na vifo na uharibifu kutokana na kimbunga Amphan nchni India na Bangladesh. Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa wale ambao wamepoteza wapendwa wao na kuwatakia waliojeruhiwa na kuathirika na kimbunga hicho, kupona haraka. 

Watu walioathiriwa na kimbunga Amphan Bengal Magharibi nchini India
© UNICEF/West Bengal IAG
Watu walioathiriwa na kimbunga Amphan Bengal Magharibi nchini India

 

Bwana Guterres amezipongeza serikali, watoa huduma za dharura na jamii kwa kazi yao ya kuwaweka watu salama kabla ya kimbunga na pia kwa kuwapatia mahitaji yao ya haraka baada ya kimbunga. 

“Umoja wa Mataifa uko tayari kuzisaidia juhudi hizi.”  Katibu Mkuu amesema kupitia ujumbe huo. 

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kwamba yuko pamoja na watu wa India na Bangladesh wakati wanapokabiliana na madhara ya kimbunga wakati huo huo wakipambana na madhara ya janga la COVID-19

Kufuatia kimbunga Amphan kilichotua nchini Bangladesh wiki hii , wilaya 19 zimeathirika na watu zaidi ya milioni 2.4 wamelazimika kuhamishiwa kwenye makazi ya muda, taarifa iliyotolewa jana na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP ilieleza.