Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa amani wa olimpiki ni kwa dunia nzima- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akutana na Rais wa Olimpiki Thomas Bach huko Pyeong Chang nchini Korea
UM/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akutana na Rais wa Olimpiki Thomas Bach huko Pyeong Chang nchini Korea

Ujumbe wa amani wa olimpiki ni kwa dunia nzima- Guterres

Masuala ya UM

Uchangamfu wa mashindano ya olimpiki ni ishara muhimu ya amani katika dunia ya leo, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres huko PyeongChang nchini Korea Kusini kunakofanyika mashindano hayo ya majira ya baridi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa michezo hiyo huku akiwa na Rais wa Kamati ya kimataifa ya olimpiki, Thomas Bach, Katibu Mkuu amesema ..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Uchangamfu utokanao na mashindano ya olimpiki huruhusu watu kuwa pamoja, kutoka pande zote za dunia, kuheshimiana na kusisitizia maadili ya stahmala, maelewano ambayo ni muhimu kwa amani kuwepo.”

Hata hivyo amesema licha ya mashindano hayo kuwa ni alama ya amani bado kwa bahati mbaya kuna mizozo mingi inaendelea huku watu wengi wakiathiriwa nayo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António akihutubia mkutano wa ufunguzi wa Olimpiki Guterres huko PyeongChang nchini Korea Kusini
UM/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António akihutubia mkutano wa ufunguzi wa Olimpiki Guterres huko PyeongChang nchini Korea Kusini
Bwana Guterres amesema ingawa kwa sasa watu wanahusisha michezo hiyo na amani kwenye rasi ya Korea, ni lazima ifahamike kuwa ujumbe wa olimpiki ni wa dunia nzima.

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Ni kwa dunia nzima. Unaheshimika Korea kama kwingineko ambako tunahaha kujaribu kushughulikia mizozo migumu ambayo tunakabiliana nayo.”

Wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, timu za Korea Kaskazini na Korea Kusini ziliingia kwa pamoja ukumbini kitendo ambacho kinaashiria amani kati ya pande mbili hizo hasimu.

Mashindano hayo yaliyoanza leo tarehe 9 yatamalizika tarehe 25 mwezi huu.