Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tujikwamue vyema tukilinda bayoanuwai baada ya COVID-19: Guterres

Samaki wa mwamba na matumbawe katika maji ya kisiwa cha Seychelles archipelago
UNDP
Samaki wa mwamba na matumbawe katika maji ya kisiwa cha Seychelles archipelago

Tujikwamue vyema tukilinda bayoanuwai baada ya COVID-19: Guterres

Tabianchi na mazingira

Kujikwamua kutoka kwenye janga la virusi vya corona au COVID-19 kunapaswa kwenda sanjari nan chi kuungana katika kulinda maliasili ya dunia hii kwa mujibu wa ahadi za kimataifa kwa lengo la kufikia mustakabali bora kwa watu wote na sayari dunia, amesema leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Katika ujumbe wake maalum wa video kwa siku ya kimataifa ya bayoanuwai ya kibaolojia Antonio Guterres amejikita katika uhusiano uliopo baina ya binadamu na viumbe vingine duniani akisistiza kwamba ulinzi na udhibiti endelevu wa bayoanuwai ni muhimu kwa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi , kuhakikisha upatikanaji wa maji na fursa ya chakula na kuzuia milipuko ya majanga.

Guterres ameongeza kuwa “COVID-19 ambayo inaighubika dunia hivi sasa imedhihirisha ni jinsi gani afya ya binadamu inahusiana kwa karibu na ulimwengu wa asili. Wakati tukiharibu maliasli na kupunguza maskani ya viumbe wengine, idadi kubwa ya viumbe vinakuwa hatarini, hii inajumuisha ubinadamu na mustakabali tunaoutaka.”

Hivyo Katibu Mkuu amesisitiza kwamba “Tunapojikwamua kutokwa kwenye mgogoro wa sasa hebu tufanyekazi Pamoja kulinda bayoanuwai ili tuweze kutimiza malengo ya maendeleo endeevu. Hivyo ndivyo tutakavyoweza kulinda afya na ustawi wa vizazi vijavyo.”

 Hali tete na tishio la maisha

Malengo ya maendeleo endelevu au SDG’s yanatoa muongozo kwa ajili ya amani ya kimataifa na ustawi ifikapo mwaka 2030.

Yanaonyesha ni kwa nini kushughulikia changamoto kama umasikini na pengo la usawa ni lazima zifanyike sanjari na kushughulikia mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira ya asili.

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema “janga la COVID-19 limezidisha ugumu wa njia za Maisha yetu, mifumo yetu ya afya na uchumi wa kimataifa. Limeongeza pengo la usawa na kutishia jamii zilizo katika hatari zaidi.”

Rais wa Baraza Kuu

Rais huyi Tijani Muhammad-Bande amesisitiza kwamba masuala haya yanauhusiano.

Ameongeza kuwa njaa tayari ilikuwa inaongezeka hata kabla ya janga la corona kukiwa na watu milioni 820 duniani kote ambao hawakuwa na chakula cha kutosha.

Uhakika wa chakula ulikuwa ukiathiriwa na kupotea kwa bayoanuwai, kuongezeka kwa hali ya jangwa na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, huku aina milioni moja za Wanyama na mimea vikikabiliwa na kutoweka.

Huku janga la corona likiendelea kuighubika dunia siku ya leo ya kimataifa ya bailojia ya bayoanuwai inaadhimishwa chini ya kaulimbiu “Suluhu zetu ziko katika asili”

Suluhu za kiasili zimeelezwa kuwa zina uwezo wa kulinda , udhibiti endelevu na kurejesha maliasili na kukarabati mfumo wa Maisha amesema Bwana. Muhamad-Bande.

“Zinaweza kushughulikia changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili na uhakika wa chakula na maji.”

Bado kuna wasaa wa kuchukua hatua

Rais huyo wa Baraza Kuu amesisitiza kwamba bado kuna muda wa kugeuza upotevu wa bayoanuwai, lakini hatua zinapaswa kuchukuliwa sasa.

Ameuelezea mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu bayoanuwai ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Septemba kuwa ni wakati muhimu wa kujenga hamasa ya kisiasa.

Wakati huohuo shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO limekuwa likibaini sukuhu za kudhibiti kupotea zaidi kwa viumbe mbalimbali.

Leo shirika hilo limefanya mkutano kupitia mtandao ili kuwasilisha ujuzi ambao umekuwa ukiundwa katika sehemu mbalimbali duniani ikiwemo kupitia mitandao yake mbalimbali na jamii za watu wa asili.

“Kutoweka huku kwa viumbe kunatutishia sote moja kwa moja, bayoanuwai sio ngeni kwetu, chakula chetu, afya na ustawi wetu vinategemea bayoanuwai. Hivyo janga hili linapaswa kutufanya tutafakari kuhusu muingiliano hu una kutegemeana huku ili tuongeze juhudi ili kwamba tuachane na njia potofu tuliyomo kwa hivi sasa.” amesema mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay.