Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maji ni sehemu ya tatizo, lakini pia sehemu ya suluhisho la mabadiliko ya tabianchi

Huko Belarus wanatumia mabwawa kama haya na kuyabadilisha yaweze kuinasa hewa chafuzi kutoka katika anga ili kuipunguza katika hewa
UNDP Belarus
Huko Belarus wanatumia mabwawa kama haya na kuyabadilisha yaweze kuinasa hewa chafuzi kutoka katika anga ili kuipunguza katika hewa

Maji ni sehemu ya tatizo, lakini pia sehemu ya suluhisho la mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Ingawa virusi vya corona au COVID-19 katika wiki za hivi karibuni vimekuwa vikichukua nafasi kubwa katika habari, hatupaswi kusahau moja ya matishio makubwa kwa ubinadamu: madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa dunia, Umoja wa Mataifa umetoa wito katika ripoti mpya kuhusu maji.

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya maji inayoadhimishwa kote duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, jumapili hii limetoa ripoti inayotaahadharisha kuwa mabadiliko ya tabianchi ytaathiri uwepo, ubora na kiasi cha maji yanayohitajika kwa matumizi na kwa hivyo kuathiri haki ya msingi ya binadamu  kwa mabilioni ya watu ya kutumia maji safi na salama ya kunywa na kujisafi.

Utafiti unaangazia kuwa kwa sasa watu takribani bilioni 2.2 wanakosa maji ya kunywa na bilioni 4.2, 55% ya idadi ya watu ulimwenguni, wanakosa mfumo wa kutosha wa kujisafi.

Hali hii inafanya kuwa vigumu, kwa mfano kufanikisha lengo namba sita kati ya malengo 17 ya Maendeleo Endelevu yaani SDGs ambayo yanaunda Agenda 2030 na ambayo inatafuta kuuuhakikishia ulimwengu upatikanaji wa maji kwa gharama nafuu kufikia mwaka 2030 na hivyo kuweka hatarini karibia mafanikio yote.

Tweet URL

 

Kwa mujibu wa takwimu za UNESCO, matumizi ya maji yameongezeka mara sita katika karne iliyopita na yanaongezeka kwa kiwango cha asilimia moja kila mwaka. Kwa kuongezea, inazingatia kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaonekana kwa kuongezeka kwa mzunguko na kasi ya hali mbaya ya hewa kama dhoruba, mafuriko na ukame au mawimbi ya joto ambayo yatazidisha hali ya nchi mbalimbali ambazo kwa sasa zina shida na 'dhiki ya maji' na matukio hayo yatasababisha shida kama hizo katika maeneo ambayo hayajaathiriwa sana.

“Madhara mengi ya mabadiliko ya tabianchi juu ya vyanzo vya maji yatatokea katika maeneo ya kitropiki, ambako nchi zinazoendelea ndiko ziliko, ambapo madhara zaidi yanaweza kutokea katika mataifa ya visiwa vidogo, ambavyo baadhi vinaweza kufutwa katika ramani ya dunia.” Imesema UNESCO.

Guterres: Lazima tuboresha ufanisi wa matumizi ya maji

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameungana na ulimwengu kuadhimisha siku ya maji duniani ambapo katika ujumbe wake kuhusu maadhimisho haya amesisitiza kuwa utumiaji mbaya wa vyanzo vya maji utatengeneza ushindani mkali usiotabirika ambao unaweza kusababisha mamilioni ya watu kuhama au kusambaratika.

Main messages of the UN World Water Development Report 2020, Water and Climate Change

 

Bwana Guterres amesema hali hii itasababisha matokeo hasi kwenye afya na tija na itasaidia kuongeza vitisho kama vile kukosekana kwa utulivu na migogoro.

"Suluhisho liko wazi. Lazima tuongeze haraka uwekezaji katika vyanzo vya maji na miundombinu ya maji yenye afya na kuboresha ufanisi wa matumizi ya maji. Lazima tutarajie na kujibu hatari za mabadiliko ya tabianchi katika ngazi zote za usimamizi wa maji." Amefafanua Bwana Guterres.