Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto wa miaka 4 anajisiwa Somalia, UNFPA yazungumza

Wasichana wakiwa katika kibanda cha walionyanyasiwa kijinsia Mogadishu. Baaadhi wanaweza kupata ajira katika duka mama mmoja mjini humo la vitambaa.
UNICEF/Holt
Wasichana wakiwa katika kibanda cha walionyanyasiwa kijinsia Mogadishu. Baaadhi wanaweza kupata ajira katika duka mama mmoja mjini humo la vitambaa.

Mtoto wa miaka 4 anajisiwa Somalia, UNFPA yazungumza

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA limelaani vikali kitendo cha kunajisiwa kwa mtoto mwenye umri wa miaka 4 nchini Somalia.
 

Taarifa ya UNFAPA iliyotolewa leo mjini Mogadishu, Somalia, inasema kuwa mtoto huyo wa kike alifanyiwa kitendo hicho tarehe 14 mwezi huu wa Mei huko Madina mjini Mogadishu.

“Tunalaani vikali kitendo cha kunajisiwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 4. Tunalaani vikali ukatili huu wa kingono wa kutisha. Ni kwa masikitiko makubwa tunaendelea kushuhudia visa vya aina hii nchini Somalia,” imesema taarifa hiyo.

Shirika hilo limesema linasimama kwa mshikamano na familia ya mtoto huyo, “na tunatoa wito kwa mamlaka kuongeza kasi ya uchunguzi wa kisa hiki na tunatoa wito ufanyike mchakato sahihi wa kimahakama.”

Halikadhalika UNFPA imesisitiza wito wake wa kutaka kupitishwa na kuwa sheria kwa muswada wa sheria ya makosa ya ukatili wa kingono, muswada ambao imesema umesalia bungeni muda mrefu bila kupitishwa.

“UNFPA Somalia inatoa wito wa kuimarishwa kwa mifumo ya ulinzi wa wanawake na watoto ambao wameendelea kuwa hatarini kukumbwa na ukatili wa kijinsia,” imesema taarifa hiyo ikitamatisha kuwa leo na kila siku, “hebu na tutetee haki za binadamu, usalama na utu wa kila mwanamke na kila mtoto wa kike popote pale alipo.”