Serikali ya Somalia imetangaza mikakati ya kuimarisha vita dhidi ya ufisadi na kuimarisha uwazi ili kujenga taasisi ambazo zinawajibika.
Waziri wa Sheria na masuala ya kisheria wa Somalia , Hassasn Hussein Haji ametangaza hayo mjini Mogadishu wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya kupinga ufisadi, sherehe ambayo iliungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Waziri alitangaza azma ya serikali yake ya kukuza uwajibikaji na pia kufutualia ufisadi katika ngazi zote za serikali huku akitia saini kile kilichoitwa mpango wa kuanzisha mradi-PIP kati ya wizara yake na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP, wenye lengo la kuimarisha taasisi za serikali ili kupigana dhidi ya ufisadi na pia kukuza uwajibikaji.
Waziri Hussein amesema, “ tuko mbioni kuunda tume ya kupinga ufisadi, na inahitaji ofisi, na wanahitaji mafunzo katika maeneo yote.Kwa hivyo nadhani mradi huu utatuongoza kukuza taasisi hii ambayo itatuwezesha kutia saini na kuridhia mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya ufisadi.”
Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Peter de Clercq, ameipongeza serikali ya Somalia kwa juhudi zake kuboresha uwazi, uwajibikaji na vita dhidi ya ufisadi katika ofisi za umma, na pia kuihimiza kuendeleza juhudi za kuelekeza kufuata mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya ufisadi, chombo alichoita, ndiyo “pekee duniani halali kinachohusika na vita dhidi ya ufisadi ambao hadi sasa mataifa 186 yameshauridhia.”
Baada ya sherehe ya kutia saini, mkuu wa UNDP nchini Somalia, George Conway, akaeleza kuwa mradi huo mpya unairuhusu serikali ya Somalia kukabiliana kikamilifu na ufisadi.