Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICJ yamaliza utata mzozo wa mpaka kati ya Kenya na Somalia baharí ya Hindi

ICJ yatoa mwongozo wa mpaka wa majini kati ya Kenya na Somalia
ICJ
ICJ yatoa mwongozo wa mpaka wa majini kati ya Kenya na Somalia

ICJ yamaliza utata mzozo wa mpaka kati ya Kenya na Somalia baharí ya Hindi

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mahakama ya Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya haki, ICJ imefunga kesi ya kugombania mpaka wa baharini kati ya Somalia na Kenya kwa kupitisha uamuzi ambao siyo tu unatupilia mbali hoja ya Kenya huku ile ya Somalia ikiungwa mkono kwa kiasi kikubwa na majaji wa mahakama hiyo bali pia unagawa nusu eneo lililokuwa linagombewa.

Eneo hilo la pembetatu katika bahari ya Hindi lina ukubwa wa kilometa za mraba 100,000 na linadhaniwa kuwa na mafuta na gesi.

Hukumu yao leo iliyoko katika kurasa 79 imepitishwa The Hague, Uholanzi ambapo katika vipengele 6 vya kesi hiyo, majaji wamekubaliana kwa kauli moja katika vipengele 4 huku wakipishana katika vipengele 2 tu.

Kupitia taarifa ya ICJ iliyotolewa mjini The Hague, kwa kauli moja majaji wamekubali hoja ya Somalia ya kwamba hakuna mpaka wa majini kati ya Somalia na Kenya.

Halikadhalika wametupilia mbali hoja ya Somalia kuwa Kenya katika eneo hilo linalogombaniwa, imekuwa ikikiuka wajibu wake kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Ramani ioneshayo mpaka wa baharini ambao Kenya na Somalia zilikuwa zinadai kuitambua.
ICJ
Ramani ioneshayo mpaka wa baharini ambao Kenya na Somalia zilikuwa zinadai kuitambua.

Mvutano huo umekuwa kitovu cha mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi mbili hizo Jirani na kwa kipindi cha miongo minne, Kenya imekuwa inasema upande wa mashariki ambako nchi hizo zinakutana kwa upande wa pwani ndio mpaka wa majini huku Somalia ikidai mahakamani kuwa mpaka wa majini unapaswa kufuata mpaka wa ardhini.

Awali Kenya ilishasema kuwa haitakubali uamuzi wowote utakaotolewa leo kwa madai kuwa ICJ imekuwa na upendeleo, na tayari Mahakama hiyo imesema uamuzi wa leo ni wa mwisho na hakuna fursa ya kukata rufaa.

Kwa uamuzi wa leo, Mahakama imegawa nusu eneo linalogombaniwa na kwa taarifa ya kuwa Kenya haitokubali uamuzi huo, bado haijafahamika mwelekeo utakuwa ni upi.

ICJ ni moja ya vyombo vikuu vya Umoja wa Mataifa na moja ya majukumu yake ni kutatua migogoro ya mipaka baina ya nchi wanachama wa Umoja wa huo.