Vyombo vya habari Tanzania vyachukua hatua kuendelea na kazi hata katikati ya COVID-19

1 Mei 2020

Ikiwa bado tunamulika harakati za vyombo vya habari kuendelea kupasha umma habari katika zama hizo za mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, nchini Tanzania vyombo vya habari navyo vimechukua hatua kuhakikisha vinaendelea kuhabarisha, kuburudisha na kuelimisha jamii licha ya kuwepo kwa mlipuko huko.

Mathalani  kituo cha televisheni cha Channel 10 ambacho ni washirika na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa au UNNews Kiswahili, katika ofisi zake zilizo jijini Dar es salaam, kumewekwa miundombinu ya kuhakikisha wafanyakazi wananawa mikono kisha wanapimwa kiwango cha joto kabla ya kuingia studio. Albert Kilala anafafanua zaidi.

“Natangaza kipindi cha asubuhi, cha Baragumu Live. Kipindi kinachohusiana na matukio ya kila siku. Tunazungumzia masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na kuhusiana na mada kuu ya siku. Tupo katika kipindi kigumu cha ugonjwa wa COVID-19 unaosabishwa na virusi vya Corona. Katika hali hii inatupasa kualika wageni kwa kutumia teknolojia ya video au video call ili tuzungumze nao na studioni huwa niko na Virda Roy.”

Hali ni vivyo hivyo kwa kituo cha radio washirika cha Storm FM kilichoko mkoani Geita nchini Tanzania kama wanavyoelezea watendaji wake.

Ibrahim ambaye pia ni mtangazaji anasema

Wengine wetu inabidi mtu afanyie kazi nyumbani kwake na kututuma kazi kwenye  barua pepe yaani email  tumekuwa tukifanya kazi kwa mfumo huo.Vilevile tukija kwenye vipindi ambavyo vinaenda hewani moja kwa moja tumebadilisha utaratibu kwa vile vipindi vyetu vingi vilikuwa vinajumuisha mahojiano ya moja kwa moja na watu mbalimbali.Kwa kuzingatia hali hii ya kutochangamana tumekuwa tukitumia teknolojia ya tihama na kufanya mahojiano kutumia simu na kutuma maswali kwa njia ya barua pepe  na wao kujibu kwa njia ya sauti kwenye simu.Imekuwa ni funzo kubwa kwetu kujua umuhimu wa teknolojia.

Naye mwenzake Zubeida ameendelea kusema.

Tangu kutokea kwa mlipuko huu wa Corona tumekuwa na mabadiliko makubwa sana haswa  kwenye dawati la michezo pia na kikubwa zaidi katika kujumuisha watu kwenye kipindi.Kwa mfano tumekuwa na kipindi cha kivumbi ndani  hii inawajumuisha watu kuanzia watano au sita hadi saba  wakiwa wanabishana kuhusiana na michezo mbalimbali.Kutokana na janga hili la Corona segment hiyo tumeisitisha kwa vile mikutano imepigwa marufuku. Badala yake tumeweka makala ambayo  tuneweza pia kujumuisha watu kwa njia ya simu na jumbe fupi fupi na kwendelea kuwaweka wasikilizaji pamoja nasi na  kupashana habari za kimichezo.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter