Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania kutangaza msimamo wake kwa UN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya UM. (Picha:UM/Joseph Msami)

Tanzania kutangaza msimamo wake kwa UN

Amani na Usalama

Tanzania itatumia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kutangaza msimamo wake na chombo hicho chenye wanachama 193. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

Msimamo wa Tanzania umetolewa na Waziri wake wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, siku ambayo taifa hilo linawasilisha hotuba yake ya mwaka.

Balozi Mahiga ambaye amemwakilisha Rais John Magufuli kwenye mkutano huo amesema..

“Rais wangu ameniambia nimwakilishe lakini pia kumuhakikishia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwamba Tanzania tutaendelea kuwa wanachama waaminifu. Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa mengine kuleta maendeleo endelevu. Ameagiza pia kwamba Tanzania itaheshimu mikataba yote ambayo imo katika Umoja wa Mataifa na ile inayogusa masuala ya kikanda, na kwamba msimamo wetu, kwanza, ni kuhakikisha maendeleo yetu yanaenda sambamba na mwelekeo ya Umoja wa Mataifa”

Waziri huyo akaenda mbali zaidi kuhusu kile ambacho Rais Magufuli amemwelekeza wafanye wakati wa jukwaa hilo..

“Tutumie kila njia na kila fursa ya kuweza kupata wadau ambao watakuwa na sisi ambao kwanza watatuelewa mwelekeo wetu katika siasa yetu katika siasa yetu katika masuala mbalimbali, tuyaeleze watu watuelewe, tuyatetee pale inapobidi, lakini kikubwa ni kuhakikisha kwamba uanachama wetu ndani ya umoja wa mataifa kama ilivyokuwa huko nyuma tangu enzi za hayati Mwalimu Julius Nyerere ni kwamba kwanza tutambulike  kama Taifa na pili tueleweke ni nini tunataka kufanya na tatu tuhakikishe kwamba, kutokana na Umoja wa Mataifa na mashirika yake na wadau wote ambao wanahudhuria kikao hiki kinachotokea mara moja kwa mwaka tunaendeleza urafiki uliopo na mataifa mbalimbali ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kuendelea kuisaidia Tanzania kama wadau wetu wa maendeleo”

Historia ya Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa inaanzia tarehe 14 Disemba mwaka 1961 wakati iliyokuwa Tanganyika ilijiunga na chombo hicho na baadaye kuungana na Zanzibar na kuwa Tanzania mwaka 1964.

Taifa hilo la Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa limekuwa likitoa hifadhi kwa wakimbizi kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC .