Wawakilishi ni nguzo ya usongeshaji wa misingi ya UN - Guterres

25 Aprili 2020

  Hii leo ni siku ya kimataifa ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao kwenye Umoja wa Mataifa, ikiwa ni maadhimisho ya kwanza tangu kupitishwa kwa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa namba 73/286 tarehe 2 mwezi Aprili mwaka 2019.

Hii leo ni siku ya kimataifa ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao kwenye Umoja wa Mataifa, ikiwa ni maadhimisho ya kwanza tangu kupitishwa kwa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa namba 73/286 tarehe 2 mwezi Aprili mwaka 2019.

Katika ujumbe wake kwa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema maadhimisho haya yanafanyika wakati ambapo ushirikiano wa kimataifa unahitaijka zaidi kuliko wakati wowote ule

“Janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 linataka hatua kutoka nchi zote, bila unyanyapaa na uzingatiaji zaidi wa wale walio hatarini zaidi,” amesema Katibu Mkuu.

UN Photo/Jean-Marc Ferré
Bendera za mataifa mbalimbali katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi.

Ameongeza kuwa mabalozi ambao wanawakilisha nchi zao kwenye Umoja wa Mataifa sasa wanakabiliana na changamoto hiyo kwa kupitisha mbinu mpya za kufanya kazi huku wakijenga tamaduni thabiti ya mazungumzo na ushirikiano.

Katibu Mkuu Guterres amesema anatumaini kuendeleza ushirikiano na wawakishi hao “wakati huu ambapo tunahaha kuokoa maisha, kupunguza machungu yanayokabili binadamu na kujenga dunia yenye amani, endelevu na yenye usawa kwa wote.”

Siku ya kimataifa ya wawakilishi inaendana na siku ya kwanza ya mkutano wa San Francisco unaojulikana pia kama Mkutano wa Umoja wa Mataifa mashirika ya kimataifa uliofanyika tarehe 24 Aprili mwaka 1945 huko San Francisco nchini Marekani.

Katika siku ya kwanza ya mkutano huo,  wawakilishi kutoka mataifa 50 walikutana baada ya madhila ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kwa lengo la kuanzisha chombo cha kurejesha amani naa kuweka kanuni za kufuatwa duniani baada ya vita hivyo kumalizika.

Wajumbe 850 walishiriki mkutano huo uliofanyika kwa miezi miwli wakiwa ni wawakilishi wa zadi ya asilimia 80 ya wakazi wa dunia wakati huo.

Tarehe 26 mwezi Juni mwaka 1945, yaani miezi miwili baada ya mkutano huo wa kwanza, Katiba au Chata ya Umoja wa Mataifa ilitiwa saini na wawakilishi wan chi 50 walioshiriki mkutano huo.

Makubaliano hayo yaliwezesha kuundwa kwa Umoja wa Mataifa ambao sasa una wanachama 193 na ni jukwaa la kimataifa la mazungumzo baina ya wawakilishi wa nchi wanachama.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud