Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani ni jukumu la kila mtu si serikali au marais pekee - UN

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akiwa kwenye sherehe ya kila mwaka ya kugonga kengele ya amani kwenye makao makuu ya UN jijini New York. Marekani.
UN /Manuel Elias
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akiwa kwenye sherehe ya kila mwaka ya kugonga kengele ya amani kwenye makao makuu ya UN jijini New York. Marekani.

Amani ni jukumu la kila mtu si serikali au marais pekee - UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, amezungumza katika tukio la upigaji wa kengele ya amani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, na kusisitiza kuwa kudumisha amani ni jukumu la kila mtu na si serikali au marais pekee.

Ingawa hivyo amesema anasikitika sana vile amani inashambuliwa hata katika fikra za watu, jamii, nchi na maeneo kupitia kauli za chuki na habari potofu na za uongo na kutumbukiza mamilioni ya watu kwenye vita huku haki za binadamu, ulinzi na ustawi vikisambaratishwa.

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema bado kuna fursa ya kurejea kwenye mwelekeo sahihi kwa kuboresha amani na kutatua changamoto zinazokabili dunia kama vile, umaskini, njaa, ubaguzi na ukosefu wa usawa. 

Ingawa tunaenda mrama, kuna fursa ya kurejesha ‘chombo’

Vile vile Guterres amesema kwamba, teknolojia inafaa idhibitiwe kwa uangalifu ili kuhakikisha kuwa ubinadamu unazingatiwa, na si kudhurika na changamoto kama vile mabadiliko ya tabianchi, uchafu wa mazingira na upotevu mkubwa wa viumbe hai.

Katibu Mkuu katika mwito wake wa amani, amewarai binadamu wazingatie zana zinazounga mkono uaminifu na mshikamano wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na tamko la Kimatiafa la Haki za Kibinadamu na Chata ya Umoja wa Mataifa.

Ameongeza pia kusongesha amani ni pamoja na kushughulikia ubaguzi wa aina mbalimbali ukiwemo wa rangi, kufanikisha Malengo ya Maendeloe Endelevu, pamoja na kupanua fursa ya usawa kwa wanawake na wasichana.

Amani tuondokane na uraibu wa nishati kisukuku

Guterres amesema kuwa, wito wa amani unamaanisha kuharakisha hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kukomesha uraibu wa nishati ya visukuku na kuwekeza katika nishati mbadala, ili kukuza sayansi badala ya porojo, uongo na chuki bila kusahau kuwaunga mkono wanaharakati, vijana na wazee, katika wito huu wa maendeleo na amani.

Tukio la kugonga kengele ya amani huenda sambamba na maadhimisho ya siku ya amani duniani, ambayo huadhimishwa tarehe 21 mwezi Septemba, lakini imeadhimiwa mapema kabla ya tarehe hiyo kutokana na taratibu za kiulinzi kuelekea kuanza kwa vikao vya ngazi ya juu kwenye makao makuu ya UN tarehe 18 mwezi huu wa Septemba.