UN na wadau watoa ombi la dola milioni 267.5 kusaidia Kenya kukabiliana na COVID-19

10 Aprili 2020

Serikali ya Kenya, Umoja wa Mataifa na wadau wake wa masuala ya kibinadamu wametoa ombi la dharura la dola milioni 267.5 kwa ajili ya kukabiliana na mahitaji ya sasa na ya dharura kwa zaidi ya watu milioni 10. 

Ombi hilo liliotolewa jijini Nairobi, Kenya linalenga kuchagiza ufadhili wa dharura kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia katika kusaidia serikali kukabiliana na mlipuko wa wa ugonjwa wa virusi vya corona au COVID-19.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya imesema fedha hizo zitakazotumika kwa kipindi cha miezi 6 ijayo, ni kwa ajili ya utoaji wa huduma ya afya ya umma ili kudhibiti kuenea kwa janga la COVID-19 nchini Kenya na kutoa msaada wa kibinadamu na ulinzi kwa jamii zilizo hatarini zaidi.

Umoja wa Mataifa umetenga dola milioni 45 kutoka mfuko wa maendeleo kwa Kenya mwaka 2018 hadi 2020 ili kusaidia kukabili COVID-19 na pia umepeleka zaidi ya wafanyakazi 70 na wafanyakazi wa kujitolea ili kusaidia serikali ya Kenya.

Mlipuko wa COVID-19 umekumba Kenya wakati tayari kuna ongezeko la mahitaij ya kibinadamu kutokana na ukame wa mara kwa mara, mafuriko yanayoendelea na uvamizi wa nzige wa jangwani.

Mwitikio wa mashirika ya Umoja wa Mtaifa na yale ya kiraia umelenga kuokoa maisha na kuzuia upotezaji wa riziki.

Kando na mahitaji ya dharura ya sasa ombi hilo litatoa kipaumbele kwa uwasilishaji wa huduma muhimu pamoja na ulinzi wa vyanzo vya kipato na msaada wa chakula kwa jamii zilizo hatarini.

Mathalani kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya, elimu, kinga, huduma kwa watoto, wanawake na jamii zilizo katika mazingira hatarishi, pamoja na watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, VVU, wakimbizi, watu waishio makazi ya watu wengi mijini manusura wa mafuriko na waathiriwa wa baa la nzige.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ombi hilo, Siddharth Chatterjee, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya amesema,

"Tutashikamana na serikali na watu wa Kenya katika vita dhidi ya COVID 19,” na kuongeza kwamba, "ombi hili la dharura ni ishara ya wazi ya mshikamano wetu tunapochagiza msaada ili kuharakisha mwitikio wetu wa kukabiliana na  COVID-19 nchini Kenya sanjari na Serikali,".

Mwendelezo wa operesheni za kibinadamu utakuwa muhimu na utategemea msaada kutoka kwa serikali kwa ajili ya usafirishaji wa misaada  wakati huu ambapo shughuli nyingi zimesitishwa.

Jamii ya kimataifa itazingatia mipango iliyowekwa na serikali kwa ajili ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona na watu waliozinatia mahitaji ya karantini na wenye vifa vya kinga ndio wataotumwa kutekeleza kazi hizo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud