Kwa watoto wa Syria miaka 9 ya mzozo ni sawa na kuwepo jehanam- Unicef

15 Machi 2020

Takribani watoto milioni 4.8 wamezaliwa nchini Syri tangu mapigano yaanze nchini humo miaka 9 iliyopita, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Kupitia taarifa yake ilyotolewa leo katika miji ya Amman, Jordan na New York, Marekani, UNICEF imesema watoto wengine milioni 1 wamezaliwa kwenye nchi jirani ya Syria wakiwa wakimbizi baada ya wazazi wao kukimbia mapigano nchini humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore ambaye wiki iliyopita amezuru Syria amenukuliwa kwenye taarifa hiyo akisema watoto hao wanaendelea kukabiliwa na madhara ya vita na kwamba, “vita nchini Syria hii leo vinatimiza historia nyingine ya aibu.”

Ameongeza kuwa mzozo huo wa Syria ukiingia mwaka wa 10, mamilioni ya watoto wanaingia muongo wa pili wa maish yao wakiwa wamezingirw ana vita, ghasia, vifo na kufurushwa na kwamba, “hitaji lao la amani sasa ni muhimu kuliko wakati wowote ule.”
Kwa mujibu wa takwimu zilizothibitishwa tangu ufuatiliaji rasmi uanze mwaka 2014, hadi 2019, zaidi ya watoto 9,000 waliuawa au kujeruhiwa kwenye mzozo huo na kwamba takribani watoto wengine wakiwa na umri wa hadi miaka 7 walitumikishwa kwenye vita. Halikadhalika takribani maeneo 1,000 ya elimu na matibabu yalishambuliwa.
UNICEF inasema kuwa takwimu hizo zikiwa zimethibitishwa, ni dhahiri kuwa madhara ya vita hivyo kwa watoto yanaweza kuwa makubwa zaidi.

“Zahma ya Syria ni moja ya janga kubwa zaidi duniani. Ghasia na mzozo huu kwa machungu zaidi vinaendelea maeneo mbalimbali ya Syria ikiwemo kaskazini-magharibi mwa Syria ambako vimeleta madhara makubwa kwa watoto, huku maeneo mengine angalau watoto wanaweza kuishi tena maisha yao ya utoto taratibu wakijenga maisha yao.” amesema Ted Chaliban Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.

Chaliban ambaye aliambatana na Bi.Fore nchini Syria amesema ni dhahiri kuwa hata hivyo, miaka 9 ya vita imetumbukiza nchi hiyo kwenye giza. Amesema kuwa, “familia zinatueleza kuwa katika hali mbaya zaidi hazikuwa na njia zaidi ya kupeleka watoto waokufanya kazi au kuoza mapema watoto wao wa kike. Hakuna mzazi ambaye analazimishwa kufanya uamuzi huo.”

Huko kaskazini-magharibi mwa Syria, takribani watoto 28,000 kutoka zaidi ya mataifa 60 wanasalia kuhaha kwenye kambi, wakinyimwa huduma za msingi. Ni watoto 765 ambao wamerejeshwa kwenye ncih zao za awali hadi mwezi Januari mwaka huu.

Ikimulika madhara zaidi ya vita hivyo vya Syria, UNICEF inasema kuwa, shule mbili kati ya tano haziwezi kutumika kwa kuwa zimeharibiwa, zimeshambuliwa au zinatumiwa kama makazi ya wakimbizi au kijeshi.

Zaidi ya nusu ya vituo vya afya havifanyi kazi huku watoto zaidi ya milioni 2.8 hawako shuleni nchini Syria au nchi jirani.

UNICEF inaongeza kuwa zaidi ya theluthi mbili ya watoto wenye ulemavu wa viungo au akili wanahitaij hudum amuhimu ambazo hivi sasa hazipo nchini Syria.

Bei za bidhaa muhimu zimepanda mara 20 tangu vita vianze mwaka 2011.
Ni kwa mantiki hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF anasema kuwa, “pande kinzani na wale wanaowaunga mkono wameshindwa kumaliza zahma hii nchini Syria. Ujumbe wetu uko dhahiri, acheni kushambulia shule na hospitali. Acheni kuua watoto. tuwezesheni kuvuta maeneo ya mapigano na mpaka ili tuweze kufikia wale wenye uhitaji. Watoto wengi wameumia kwa muda mrefu.”

Kwa sasa UNICEF inashirikiana na wadau wake nchini Syria na nchi jirani kuwapatia msaada watoto ambapo mwaka jana pekee mathalani UNICEF imepatia chanjo watoto 750,000 dhidi ya surua. Zaidi ya watoto milioni 1 walipatiwa msaada wa kisaikolojia ilhali watoto milioni 3 walipatiwa elimu rasmi na isiyo rasmi.

Hata hivyo kwa sasa UNICEF imesema inahitaji dola milioni 682 ili iweze kusongesha huduma hizo muhimu hasa kwa kuzingatia kuwa hivi sasa inakabiliwa na ukata.

Shirika hilo limekumbusha hata hivyo kuwa suluhu pekee Syria si misaada ya kibinadamu bali kumaliza mzozo kwa njia ya kidiplomasia.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud