Dola milioni 621 zasakwa kusaidia wakimbizi na wenyeji DRC

6 Machi 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wake huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wanaomba dola milioni 621 ili kusaidia raia wa taifa hilo waliosaka hifadhi nchi jirani sambamba na wale wanaowahifadhi.

Ombi hilo lililopatiwa mpango wa usaidizi wa kikanda kwa wakimbizi kwa mwaka 2020-2021, limezinduliwa leo huko Geneva, Uswisi likijumuisha shughuli za kibinadamu zinazoendeshwa na mashirika 66 ili kulinda wakimbizi na kuwasaidia kujenga maisha yao kule walikosaka hifadhi.

Maeneo walikosaka  hifadhi wakimbizi kutoka DRC ni pamoja na Uganda ikihifadhi idadi kubwa ya wakimbizi hao takribani 400,000. Wengine wako Burundi zaidi ya 84,000, Tanzania na Rwanda kila moja ikihifadhi zaidi ya wakimbizi 75,000 wa DRC, Zambia wakimbizi 50,000, Angola 23,000 na Jamhuri ya Congo, 21,000).

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva kuhusu ombi hilo, msemaji wa UNHCR, Babat Baloch amesema mzozo wa DRC unasalia kuwa moja ya majanga ya muda mrefu zaidi ya kibinadamu barani humo na kwamba, “rasilimali za dharura zinahitajika kusaidia nchi za Kusini mwa Afrika na Maziwa Makuu ambazo zinahifadhi zaidi ya wakimbizi na wasaka hifadhi 900,000 kutoka DRC. Wakimbizi hawa wanasaka usalama kwenye maeneo ambako jamii za wenyeji tayari zimekumbwa na uhaba wa rasilimali.”

 UNHCR inasema kuwa ijapokuwa kipindi cha mpito cha kubadilisha serikli kilifuatiwa na uchaguzi wa rais mwezi Desemba mwaka 2018, hofu bado imesalia juu ya kuzorota kwa hali ya kibinadamu na usalama, hususan kwenye maeneo ya mashariki mwa DRC.

Bwana Baloch amesema, “mzozo wa kivita umeshamiri mashariki mwa DRC katika miaka iliyopita na mapigano ya kikabila, vinaendelea kufurusha wakongo ndani ya nchi yao na wengine kuvuka mipaka.”

Amesema DRC ina zaidi ya wakimbizi aw ndani milioni 5 ambao wengine wao wamelazimika mara kadhaa kukimbia makazi yao kutokana na mapigano mathalani huko Ituri, Kivu Kusini na Kivu Kaskazini.

Amekumbusha kuwa ombi la kipeke yake lilizinduliwa hivi karibuni kusaidia shughuli za kibinadamu DRC likilenga watu milioni 8.1 katika taifa hilo ambalo lenyewe lina wakimbizi zaidi ya 500,000 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.

Bwana Baloch amesema wakati wanatoa ombi jipya kwa mwaka 2020-2021, lile la mwaka jana wa 2019, la dola milioni 720 lilifadhiliwa kwa asilimia 22 pekee.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter