Hali inazidi kuwa mbaya kwa waliotawanywa na machafuko DRC:UNHCR

11 Februari 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linatiwa wasiwasi mkubwa na kuendelea kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini Jamhuroi ya Kidemokrasia ya Congo DRC hasa eneo la Mashariki kwenye jimbo la Beni.

Kwa mujibu wa shirika hilo machafuko ya karibuni katika jimbo la Beni yamewalazimisha zaidi ya raia 100,000 kuzikimbia nyumba zao katika muda wa miezi nmiwili iliyopita.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis na msemaji wa shirika hilo Andrej Mahecic inasema mashambulizi ya makundi yenye silaha tangu Desemba mwaka jana kwenye miji na vijiji vya utawala wa kichifu wa Watalinga karibu na mpaka wa Uganda yamewatawanya wanawake, wanaume na watoto na wengi wamekimbilia katika mji wa Nobili na viunga vyake.

UNHCR inasema “wengi wa watu hawa waliotawanywa tayari walifurushwa na machafuko ya awali na walikuwa ndio wamerejea tu vijijini kwao mwezi Novemba mwaka jana baada ya kukimbia machafuko ya April na wanahitaji haraka msaada wa kibinadamu.”

Hof una mvutano katika eneo hilo vimeongezeka tangu serikali ilipozindua operesheni za kijeshi mwezi Desemba dhidi ya wapiganaji wa ADF.

Takribani raia 252 wanakadiriwa kuuawa jimboni Beni tangu Desemba mwaka jana na watu wengi wamewaeleza wafanyakazi wa UNHCR kwamba sasa wanaishi kwa hofu kubwa baada ya kushuhudia mauaji, ukatili wa kingono na utekeji majumbani na wakati wa vita.

Watu wengi waliotawanywa na machafuko ya karibuni wanapata hifadhi Nobili na wengine katika shule na makanisa yaliyofurika katika viunga vya mji wa Nobili. UNHCR na washiriska wake wanawapatia msaada msaada ikiwemo malazi ya dharura na pia kusaidia shule kurejea katika masomo.

Mbali ya msaada wa malazi , chakula, huduma za afya, maji na vifaa vingine vya muhimu UNHCR inasema watu hao wanahitaji ulinzi.

Watu zaidi ya milioni 5 wametawanywa DRC na kuifanya nchi hiyo kuwa na idadi kubwa Zaidi ya wakimbizi wa ndani barani afrika. Sasa UNHCR inahitaji dola milioni 150 mwaka huu ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani lakini kiasi ilichopokea hadi sasa ni asilimia 4 tu ya fedha hizo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter