Wakimbizi zaidi ya 500 wa DRC wasaka hifadhi Uganda

Machafuko katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC yansababisha watu kukimbilia nchi jirani.
UNICEF/Madjiangar
Machafuko katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC yansababisha watu kukimbilia nchi jirani.

Wakimbizi zaidi ya 500 wa DRC wasaka hifadhi Uganda

Wahamiaji na Wakimbizi

Watu zaidi ya 500 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wamelazimika kusaka hifadhi katika nchi jirani ya Uganda kufuatia mapigano mapya yaliozuka juma lililopita nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. 

UNHCR imesema idadi ya wanaokimbia inaongezena na kwamba kwa sasa angalau wakimbizi 70 wanapokewa kwenye mapokezi ya wakimbizi ya Sebagoro wilayani Kikuube kwa siku.

Duniya Aslam Khan, Msemaji wa UNHCR nchini Uganda amesema wanashirikiana na mamlaka za serikali ya Uganda kuwachekecha na kuwasafirisha hadi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kyangwali umbali wa karibu kilomita 30.

Walifungasha virago wakati wananchi walikuwa wakijiandaa kusherelekea siku ya mwaka mpya inayoshangiliwa sana nchini DRC marufu kama ‘Bon ane’ ambapo wapiganaji wa Kilendu na Wagegere walianza kukabiliana na kushambulia vijiji wilayani Bunia.

Kulingana na simulizi za wasaka hifadhi hao, maeneo yalioathiriwa zaidi na mapigano ya siku kuu ni pamoja na Joo, Muvaramu, Mkpi, Tara na Roo.    

Kamishina wa wilaya ya Hoima Samuel Kisembo amesema wameimarisha usalama mpakani pamoja na kuwachekecha ebola ili kuzuia maambukizi ya maradhi hayo hatari na uwezekano wa wanamgambo kujipenyeza nchini Uganda chini ya mwavuli wa wakimbizi.

Kulingana na UNHCR Tangi Desemba 2018, wakimbizi zaidi ya 18,000 kutoka DRC, wameingia Uganda kwa usafiri hatari wa boti zikiwemo zile za uvuvi kuvuka Ziwa Albert.

Wameingia wakati ambapo UNHCR unakumbana na pengo la ufadhili lililosababisha ukata wa msaada kwa wakimbizi wengi hasa wale waliowasili kabla ya miaka miwili iliopita. Mwaka jana lilipokea ufadhili wa dola milioni 147 kati ya dola bilioni 1.03 lilizoomba kusaidia wakimbizi mwaka huo wa 2019.