Wakimbizi na wenyeji wakilima pamoja ni faida kwa jamii nzima:UNHCR 

3 Disemba 2019

Mradi wa pamoja wa kilimo ulioanzishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, umekuwa nuru inayowaangazia wageni ambao ni wakimbizi na jamii za wenyeji kwa kuwafanya wote kuweza kujitegemea mfano Neema Amayo mkimbizi kutoka Sudan Kusini aliyewasili Kaskazini mwa DRC na watoto watano bila chochote. 

Katika eneo la Biringi iimbo la Ituri DRC, Wahenga hawakukosea kunena kuwa jembe halimtupi mkulima na ndiyo ilivyokuwa kwa mkimbizi Neema Amayo ambaye kilimo limebadili maisha yake.  Alikimbia vita Sudan Kusini na kuingia DRC na wanae baada ya vita kumgharimu kila kitu. Sasa hapa ameaanza maisha upya na anasema, “tunalima vitu vingi, kabeji, nyanya, mabiringanya na mchicha. Tunakuja hapa shambani  kufanyakazi kila siku na kwa matunda ya jasho letu  tunaweza kuvuna na kuuza mazao yetu sokoni. Tunaweza kuishi maisha mazuri, na kuendelea na maisha yetu kama kawaida.”

Jamii za wenyeji zilitoa ardhi na faida inayopatikana wanagawana na Neema na wakimbizi wengine. Msimu huu  wamevuna zaidi ya kilo 7,000 za mbogamboga . Guillaume Mageu Bhangra ni chifu wa eneo hilo ambaye anasema kuwa, “ kama chifu wa eneo hili ninafurahi sana kuona wakimbizi wanalima ardhi yetu ili kuweza kuishi na kujilisha. Hivyo ninapokuja hapa na kujionea mavuno haya imekuwa vizuri sana na inanipa furaha kubwa. Mkimbizi hapaswi kuteseka katika nchi yetu ambayo inawahifadhi.”

DRC inahifadhi takriban wakimbizi 100,000 kutoka Sudan Kusini. UNHCR na wadau wake wanawapa wakulima kama Neema mafunzo, mbegu na nyenzo za kilimo. Neema anakumbuka alivyowasili akisema kuwa, “nilikuja hapa peke yangu bila mume bali na watoto wangu wote . Na nilipowasili ilikuwa vigumu kuisha hususan na watoto , wakati mwingine hatukuwa na chakula cha kutosha. Tangu nilipoanza kulima ninaishi vizuri. Sasa naweza kununua viungo na hata sabuni , ni muhimu kwa sababu nitaweza kuhudumia familia yangu.”

Sasa Neema amepata si tu usalama, bali jamii na mahali pa kujenga upya maisha yake na ya familia yake.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter