Dola milioni 877 zahitajika kusaidia warohingya mwaka 2020

3 Machi 2020

Umoja wa Mataifa na washirika wake leo wamezindua ombi la pamoja la kuchangisha dola milioni 877 ili kushughulikia janga la wakimbizi wa Rohingya na jamii zinazowahifadhi nchini Bangladesh.

Ombi hili kwa mwaka huu wa 2020 linalenga kuimarisha juhudi za awali za kusaidia wakimbizi hao wapatao 855,000 kutoka Myanmar na wenyeji wao wabangladesh zaidi ya 444,000.

Asilimia 55 ya fedha hizo zinalenga huduma muhimu na misaada ikiwemo chakula, malazi, maji safi na salama, huduma za kujisafi ambapo chakula pekee ni asilimia 29.

Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lile la wahamiaji, IOM wakizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo wamesema kuwa afya, ulinzi, elimu, usimamizi wa makazi ya warohingya, nishati na mazingira vinaendelea kuwa muhimu katika kuhakikisha usalama na utu wa wakimbizi hao sambamba na wenyeji wao.

Kwa mujibu wa UNHCR, mwaka 2020 ni miaka mitatu tangu wakimbizi hao wakimbilie Bangladesh na ni dhahiri shahiri kuwa warohingya wanataka kurejea nyumbani.

Akizungumzia ombi hilo, Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema kuwa kuunga mkono ombi hilo,“ni muhimu ili kulinda ustawi wa wakimbizi wa kabila la Rohingya, walioko Bangladesh na pindi itapokuwa salama kwa wao kurejea nyumbani Myanmar. Hadi wakati huo, dunia inapaswa kushikamana na warohingya na serikali na watu wa Bangladesh wanaoendelea kuwahifadhi. Jambo muhimu tutaendelea kushirikisha wakimbizi na kusikiliza sauti zao na kuelewa matumaini yao na dira yao ya baadaye.”

Akifafanua kuhusu  uwazi katika suala la uraia, Bwana Grandi amesema kuwa, “uwazi huo ni kwa mujibu wa kamisheni kama ile iliyoundwa na wajumbe walioteuliwa na Umoja wa Mataifa ambapo wakimbizi wanapaswa kuelewa uraia una maana gani, ili wasiweze kubaguliwa na ili hatimaye waweze kutangamana kwa ukamilifu kwenye nchi yao na jamii zao.”

Mmiminiko wa wakimbizi Bangladesh na huduma za kuhifadhi mazingira

Miezi na miaka iliyofuatia kukimbia kwa warohingya kutoka jimboni kwao Rakhine nchini Myanmar, Bangladesh na wananchi wake, wameshuhudia wakiendelea kuhifadhi wakimbizi wa kabila la Rohingya kwenye kambi zilizopo kusini-mashariki mwa taifa hilo la Asia kwenye eneo liitwalo Cox’s Bazar.

Akizungumzia umuhimu wa kuendelea kwamsaada wa kimataifa kwa Bangladesh, NAibu Waziri a Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Shahriar Alam, amesema kuwa warohingya takribani  nusu milioni waliingia Bangladesh katika siku 17 za mwanzo kabisa wa zahma yao mwezi Agosti mwaka 2017.

Ombi hilo la pamoja linaweka msisitizo kwenye maeneo ambayo yameathiri zaidi jamii wenyeji ikiwemo miundombinu ya huduma za umma na kupata  huduma za umma, njia endelevu za kujipatia kipato, kuhifadhi mazingira na upatikanaji wa nishati.- UNHCR, IOM

Bwana Alam amesema kuwa, “tunatarajia kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zitachukua hatua zaidi na kushirikiana nami kwa kadri zinavyoweza ili kushinikiza Myanmar kuwarejesha raia wake nyumbani kwa usalama, kwa hiyari na kwa njia ya kiutu.”

Kwa mujibu wa UNHCR, IOM na Bangladesh, ombi la mwaka huu wa 2020 linaweka msisitizo zaidi katika kusaidia jamii za wenyeji ambazo zimewachukua wakimbizi warohingya na kuwasaidia.

Hivi sasa kaya za warohingya zina gesi ya kupikia ambayo imesaidia kupunguza kwa asilimia 80 mahitaji ya kuni.

Mashirika ya UN yanasema kuwa kaya 30,000 za kibangladesh nazo zimejumuishwa kwenye mpango huo wa gesi ya kupikia kwa lengo la kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na hivyo kuhifadhi mazingira kwenye eneo la Cox’s Bazar.

Ombi hilo la pamoja linaweka msisitizo kwenye maeneo ambayo yameathiri zaidi jamii wenyeji ikiwemo miundombinu ya huduma za umma na kupata  huduma za umma, njia endelevu za kujipatia kipato, kuhifadhi mazingira na upatikanaji wa nishati.

Ombi la mwaka 2019 la dola milioni 921 lilichangiwa kwa zaidi ya asilimia 70 ambayo ni sawa na dola milioni 650.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter