Utambuzi wa warohingya huko Bangladesh waendelea

6 Julai 2018

Hatimaye warohingya wanapatiwa vitambulisho, ikiwa ni mara ya kwanza katika maisha yao. Vitambulisho hivyo ni vya ukimbizi huko Bangladesh.

Zoezi la kuthibitisha utambulisho wa wakimbizi wa kabila la Rohingya waliosaka hifadhi nchini Bangladesh linaendelea kwa ushirikiano kati ya serikali na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Kazi hiyo ilianza mwishoni mwa mwezi uliopita ambapo itasaidia kuwa na kanzi data ya wakimbizi hao na matarajio ni kuikamilisha ndani ya miezi sita.

UNHCR inasema itajumuisha takribani warohingya 900,000 waliomiminika nchini Bangladesh wakiwemo wale 700,000 ambao wameingia tangu ghasia zianze tena kwenye jimbo lao la Rakhine nchini Myanmar mwezi Agosti mwaka jana.

Kazi hiyo ya utambuzi ni muhimu kwani itasaidia kuwa na kanzi data ya kufahamu kule walikotoka Myanmar.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi Charlie Yaxley amewaambia waaandishi wa habari kuwa kazi hiyo ya utambuzi ni muhimu kwani itasaidia kuwa na kanzi data ya kufahamu kule walikotoka Myanmar.

Halikadhalika itasaidia kuwa na taarifa kamili za wakimbizi hao na hivyo kurahisisha mipango ya misaada kutoka serikali ya Bangladesh, wadau wa misaada ya kibinadamu na pia kurahisisha uratibu na hivyo kuongeza ufanisi wa usaidizi.

Bwana Yaxley anafafanua kile kinachofanyika akisema kuwa, “Utambuzi wa kama vile mboni za jicho, vidole na pia picha unatumika ili kuthibitisha utambulisho wa kila mkimbizi mwenye umri wa zaidi ya miaka 12. Baada ya hapo anapatiwa kitambulisho kipya. Kwa wakimbizi wengi hii ni mara ya kwanza wanamiliki nyaraka ya utambulisho binafsi.”

Hadi sasa takribani wakimbizi 4,200 wamepatiwa vitambulisho tangu zoezi lianze tarehe 21 mwezi uliopita ambapo mafanikio yanatokana pia na kampeni za kuhamasisha wakimbizi hao wa kabila la Rohingya kuhusu umuhimu wa nyaraka hiyo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud