Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja tangu kuanza kwa janga la warohingya: Nyumbani na ugenini kote kuchungu

Zulkhair, mwenye umri wa miaka 27, anabeba mtoto wake wa miezi 10, Mohammad, kambini Kutupalong. Mohammad ni mgonjwa na anahitaji matibabu. Picha: © UNHCR / Paula Bronstein

Mwaka mmoja tangu kuanza kwa janga la warohingya: Nyumbani na ugenini kote kuchungu

Wahamiaji na Wakimbizi

Mwaka mmoja tangu warohingya waanze kukimbia jimbo la Rakhine nchini Myanmar kutokana na mateso dhidi yao, bado Umoja wa Mataifa unashindwa kufikisha ipasavyo misaada ya kibinadamu kwa waliosalia jimboni humo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada ya dharura imesema hadi sasa kuna zaidi ya raia laki Sita na Nusu jimboni humo na 176,000 kwenye eneo la kaskazini mwa jimbo hilo.

Msemaji wa OCHA Jens Laerke amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kuwa ingawa wana nia ya kwenda kufikisha misaada ya kibinadamu inayohitajika zaidi, bado hawawezi kufika.

“ Mashirika mengi ya misaada ya kibinadamu ambayo  yamekuwa yamefanya kazi kwa miaka mingi kaskazini mwa jimbo la Rakhine bado  hayajaweza kuanza tena kutoa huduma na programu zao kwa wananchi ambao wako hatarini zaidi,” amesema Bwana Laerke.

(Picha:UNNewsKiswahili/Assumpta Massoi)
"Ugenini unapogeuka lulu"

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, likizungumzia hali ya wakimbizi warohingya waliosaka hifadhi huko Bangladesh, limetoa wito wa usaidizi zaidi.

Andrej Mahecic msemaji wa UNHCR ameeleza kuwa wakimbizi zaidi ya 600,000 wamesaka hifadhi kwenye makazi ya Kutupalong yaliyoko wilaya ya Cox’s Bazar nchini Bangladesh akisema kuwa idadi hiyo “inafanya iwe makazi makubwa na yaliyo na idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani. HIi inaongeza changamoto za kila siku za makazi, huduma za maji, huduma za kujisafi, huduma za msingi pamoja na ulinzi na usalama kwa wanawake na wasichana.”

Bwana Mahecic amesema ombi la pamoja la mashirika ya misaada la dola milioni 950.8 lililotolewa mwezi MAchi mwaka  huu wa 2018 limefadhiliwa kwa zaidi ya asilimia 33 tu.

Amesema kiwango hicho kidogo cha ufadhili kinatia wasiwasi  kwa kuwa hivi sasa wanakaribia robo ya mwisho yam waka 2018 na hivyo kuwa katika nafasi ngumu ya kuboresha mazingira ya wakimbizi warohingya na jamii zinazowahifadhi.