Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wazazi warohingya wahofia mustakabali wa elimu kwa watoto wao Cox’s Bazar

Wakimbizi wa Rohingya wakitembea katika mvua katika kambi ya Kutupalong, wilaya ya Cox's Bazara.2018
© UNHCR/David Azia
Wakimbizi wa Rohingya wakitembea katika mvua katika kambi ya Kutupalong, wilaya ya Cox's Bazara.2018

Wazazi warohingya wahofia mustakabali wa elimu kwa watoto wao Cox’s Bazar

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linafanya kila liwezalo kuhakikisha watoto wakimbizi warohingya huko Bangladesh wanapata elimu wakati huu ambapo wazazi wao wana hofu kubwa juu ya mustakabali wa elimu ya watoto hao.

UNHCR inasema kuwa zaidi ya nusu ya wakimbizi wote 620,000 warohingya kutoka Myanmar ambao wanaishi kwenye makazi ya Cox’s Bazar, kusini-mashariki mwa Bangladesh ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 18.

UNHCR inasema asilimia 39 ya watoto warohingya wenye umri wa kati ya miaka 3 hadi 14 na asilimia 91 ya vijana bado hawana fursa ya kujifunza kwenye makazi hayo yaliyojaa pomoni.

Hata hivyo UNHCR tayari imechukua hatua kwa kufungua kituo cha kujifunza kwa watoto kwenye makazi ya wakimbizi ya Kutupalong wakifundishwa hesabu, kiingereza na lugha ya Myanmar.

Walimu wao ni kutoka Bangladesh na pia Myanmar ambapo Asma Bibi ni mwalimu msaidizi ambaye ni wa kabila la warohingya na anasema,

Sauti ya Asmaa Bibi

“Kadri ninavyofundisha hawa watoto, inanisaidia nisisahau kile nilichojifunza maishani.”

Wazazi wa watoto hao wakimbizi nao pamoja na matumaini kwa kuona watoto wao wanasoma, bado wana hofu miongoni mwao ni Abu Sayed,

 Sauti ya Abu Sayed

 Tulipofika hapa tulikuta shule, na watoto wachache wakiwemo Kamal na Anjul wanasoma pale. Iwapo hawatapata elimu watakuwa wajinga. Natamani tungalikuwa na fursa kwa watoto wetu kupata elimu, hiyo itakuwa ni fursa ya kipekee.”

 

TAGS: Warohingya, Bangladesh, Cox’s Bazar, Elimu, UNHCR, Watoto