Maelfu ya watu Maisha yao yanaendelea kuwa hatarini Syria:WHO/OCHA/UNHCR

28 Februari 2020

Umoja wa Mataifa unaendelea kufuatilia kwa karibu hali inayotia hofu kubwa Kaskazini Magharibi mwa Syria kufuatia taarifa kwamba askari kadhaa wa Uturuki wameuawa kwenye shambulio la anga. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amerejelea wito wake wa kusitisha uhasama mara moja na kuokoa Maisha ya raia walio hatarini kufiuatia machafuko yanayoendelea na mashambulizi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa shirika la afya ulimwenguni WHO Christian Lindmeier amesema katika kuwasaidia raia waliojeruhiwa kwenye machafuko hayo WHO imepeleka malori yaliyosheheni tani 55 za madawa na vifaa vingine vya tiba kutoka Uturuki hadi Idleb na baadhi ya sehemu za Aleppo, “hadi kufikia leo kati ya vituo vya afya 84 vilivyolazimika kusitisha operesheni zake tangu Desemba 2019, vituo 31 kati ya hivyo vimefanikiwa kuhamishwa na kutoa huduma ambako watu wamesaka hifadhi kukimbia mashambulizi.”

Ameongeza kuwa tangu Desemba Mosi mwaka jana hadi leo kumeripotiwa mashambulizi 11 kwenye vituo vya afya Syria.

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema halijapokea mawasiliano kuhusu wakimbizi wa Syria kusafiri kutoka Uturuki kuelekea nchi za Ulaya na Kamishina mkuu wa shirika hilo Filippo Grandi ametoa wito kwa nchi za jirani ikiwemo Uturuki kupanua wigo wa kupokea wakimbizi wa Syria na kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wake kwa Uturuki ambayo tayari ilikuwa na mzigo mkubwa wa wakimbizi wa Syria.

Nayo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA kupitia msemaji wake Jens Laerke imethibitisha kwamba, “bado hakuna mawasiliano yoyote rasmi kutoka kwa serikali ya Uturuki kuhusu madai ya mabadiliko ya sera kuhusu wakimbizi wa Syria nchini Uturuki na wakati huohuo operesheni za kibinadamu mpakani baina ya Uturuki kuingia Syria zenaendelea.”

Pia amesema dola milioni 100 zimepokelewa kama sehemu ya ombi la dola milioni 500 za kutoa msaada wa kibinadamu Kaskazini Magharibi mwa Syria.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter