Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Eritrea bado yanyamazisha wapinzani- Ripoti

Huyu ni raia wa Eritrea akionyesha ngozi yake ilivyo baada ya kupata ugonjwa wa ngozi akiwa katika kituo cha kuwazuilia cha Zawiya Tripoli Libya
Picha ya UNICEF/Alessio Romenzi
Huyu ni raia wa Eritrea akionyesha ngozi yake ilivyo baada ya kupata ugonjwa wa ngozi akiwa katika kituo cha kuwazuilia cha Zawiya Tripoli Libya

Eritrea bado yanyamazisha wapinzani- Ripoti

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet, amesema hali ya haki za binadamu nchini Eritrea bado si nzuri licha ya mkataba wa kihistoria wa amani kati yake na Ethiopia mwezi Julai mwaka 2018.

Bi. Bachelet amesema hayo leo huko Geneva, Uswisi wakati akiwasilisha ripoti  ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na ripoti yake kuhusu hali ya haki za binadamu Colombia, Cyprus, Eritrea, Guatemala, Honduras, Iran, Nicaragua, Sri Lanka, Venezuela na Yemen.

“Licha ya mkataba wa amani wa kihistoria na Ethiopia, makubaliano ya ushirikiano na Djibouti, kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia na Somalia, hali ya haki za kibinadamu nchini Eritrea haijaimarika. Uhuru wa raia kufanya mambo yao bado umebinywa na serikali, haki za kujieleza, kukusanyika na imani pamoja na  uhuru wa vyombo vya habari kwa kiasi kikubwa unadhibitiwa,”  amesema Bi. Bachelet.

Amesema kinachomchukiza zaidi ni msako dhidi ya watu ambao wanaeleza kisirisiri ukosoaji wao dhidi ya serikali. “Mathalani, baada ya maaskofu wa madhehebu ya kikatoliki kutoa barua yao ya kitume ikitaka haki na marekebisho, hospitali 21 zinazosimamiwa na kanisa katoliki ziliripotiwa kufungwa. Tumepokea pia ripoti ya watu kukamatwa na kutiwa korokoroni kisa tu ni imani zao,”  amesema Kamishna Mkuu huyo wa haki za binadamu.

Amesema raia wengine wa Eritrea wamekuwa wakiswekwa ndani kwa kutekeleza haki yao ya msingi kama vile kujieleza au kuabudu ilhali wanaoswekwa ndani hawafunguliwi mashtaka yoyote na wengine wanakuwa hata hawana tena mawasiliano.

Bi. Bachelet amesema kuwa, Eritrea inapaswa kuhakikisha kuwa watu walioswekwa rumbande wanatendewa kiutu; wale waliokamatwa kiholela waachiliwe huru na kama kuna mashtaka basi wafikishwe mahakamani lakini wapatiwe haki sambamba na ieleze mustakabali wa wale ambao hadi sasa wametoweka.”

Amesema anaungana na kamatiya haki za binadamu kuelezea wasiwasi wake kuhusu ukwepaji sheria ulioenea nchini humu kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Kulikoni waeritrea wanakimbia nchi yao?

Kamishna Mkuu Bachelet amesema kuwa sababu kuu ni kipindi kisichojulikana na kigumu cha kuhudumu jeshini kwa vijana na hivyo wanalazimika kukimbia. “Baadhi ya makuruta wanatumiwa kama vibarua bila malipo. Serikali imesema kuwa kuna mipango inafanyika kwa ajili ya makuruta hao lakini hakuna mikakati ya dhati iliyochukuliwa hadi leo hii.”

Bi. Bachelet amesihi serikali ya Eritrea itangaze ratiba ya kuwaondoa vijana hao kwenye huduma hiyo isiyo na mwisho sambamba na kuruhusu kampuni binfasi ili ziweze kuanzisha ajira kwa vijana.

Amekumbusha kuwa, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa upande wake imekuwa ikitoa msaada wa kiufundi ikiwemo kwenye maeneo ya kuimarisha mahakama, haki za watu wenye ulemavu na haki za kupata maji safi na huduma za kujisafi.

Kuhusu Iran, Bi. Bachelet amenukuu ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ikisema kuwa ilhali serikal inaonyesha juhudi katika suala la adhabu ya kifo hasa kwa wafungwa watoto, bado hatua zaidi zinahitajika hasa utoaj iwa adhabu ya kifo kwa watoto.