Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Apu mpya ya IOM kuhakikisha ridhaa ya matumizi ya taarifa binafsi mitandaoni

Kijana akicheza mchezo kwenye apu ya simu.
UN News/Elizabeth Scaffidi
Kijana akicheza mchezo kwenye apu ya simu.

Apu mpya ya IOM kuhakikisha ridhaa ya matumizi ya taarifa binafsi mitandaoni

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limezindua Apu mpya ya simu za rununu ijulikanayo kama “Community Response App” ambayo inaweza kutumika kokote duniani kuwawezesha wanaosimulia hadithi zao kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya taarifa zao binafsi, kulikoni? 

Kwa mujibu wa Shirika la IOM ridhaa inahitajika kabla ya kukusanya takwimu au taarifa binafsi ikiwemo kwa njia ya picha, sauti  na video kwani kila siku zaidi ya picha milioni mbili zinapigwa kila dakika na kuchagiza mawasiliano ya kasi ya kusambaza taarifa katika majukwaa mbalimbali.

Kama waandaji wa taarifa IOM inasema wana wajibu mkubwa wa kuwawezesha watu wanaotoa hadithi zao ili waweze kufanya maamuzi bora ya jinsi gani na wapi taarifa zao binafsi zikusanywe, kuhifadhiwa na kuchapishwa

Na ili kufanikisha hilo ndio maana IOM imezindua Apu ya Community Response, ambayo “ni apu ya kipekee ya simu za rununu inayomuwezesha mtu kutoa ridhaa kwa njia ya kidijitali, akiwa mashinani, mtandaoni au hata nje ya mtandao.

Apu hiyo inaruhusu kuwapa watu taarifa za wazi kwa njia ya maingiliano na kutoa ridhaa ya kutumia taarifa binafsi  mfano picha, video na kurekodi sauti.

IOM imeongeza kuwa“Apu hiyo inatoa chaguo na muongozo wa kukusanya thibitosho la ridhaa wakati wa kufanya kazi na makundi, watoto au vijana.”

Na fomu hiyo ya ridhaa inatoa  fursa ya kukubali au kukataa kutumika kwa baadhi ya taarifa zao binafsi.

 Kwa mfano mtu anaweza kuchagua kutumika kwa sauti yake tu na kutoonyesha sura yake, hii inamaanisha kwamba mtu anaweza kudhibiti taarifa zake binafsi zinazotolewa kwa umma na fomu hiyo ni lazima iwekwe sahihi.

IOM inasema apu hii ambayo inapatikana kwa lugha mbalimbali itawarahisishia watu binafsi na mashirika kuwajibika vilivyo wakati wa kutoa hadithi halisi za watu.