Mazingira ya Libya yalikuwa tete ndio maana nikarejea nyumbani: Mhamiaji Mohamed

5 Januari 2021

Kutana na muhamiaji Mohamed Ahmed Bushara aliyekwenda kusaka maisha Libya miaka mitano iliyopita lakini hali ngumu, ubaguzi , machafuko na kuwekwa rumande vilimkatisha tamaa ya kukimbiza ndoto hiyo na akakata shauri kurejea nyumbani Sudan kushika ustaaranu mwingine kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM na Muungano wa Ulaya. 

Mohamed Bushara ambaye sasa amerejea nyumbani na anamiliki duka la vipodozi anasema anatokea eneo la Al Mawgoba na aliondoka Sudan kuelekea Libya mwishoni mwa mwaka 2016 kwa sababu hali ya kifedha ilikuwa mbaya na alitaka kwenda kufanyakazi na kusaka mustakbali bora Misrata, lakini mambo yalikuwa ndivyosivyo na ndoto yake ikaishia rumande,“Misrata Libya tulikuwa katika eneo la bvita na tulikuwa wengi sana kutoka mataifa mbalimbali na watu kutoka Sudan tulikuwa 86 na hiyo ilikuwa bado hata maigano hayajasika kasi Libya. Nilipotambua hilo nilitaka kurudi nyumbani. Mwakilishi kutoka ubalozini alikuja kukutana nami, na miongoni mwa wafungwa wote nilikuwa peke yangu niliyetaka kurejea nyumbani, wakaniambia watawasiliana na shirika moja na namshukuru Mungu waliwaleta IOM ambao waliniuliza kama nataka kurudi na wakanisaidia kufanya mipango ya kurejea nyumbani.” 

IOM walimpatia fedha za safari na kumpeleka hadi uwanja wa ndege kisha wakamsafirisha mpaka Sudan na kumwambia awasiliane na shirika hilo baada ya kuwasili. 

Na baada ya siku nne Mohammed aliwapigia simu IOM akaenda kwenye ofisi zao Al Manshiya ambako walimuuliza ni biashara gani anataka kufanya akawaambia kufungua duka la vipodozi. 

Miezi minne baadaye kupitia mradi wa pamoja wa IOM na Muungano wa Ulaya EU wa kusaidia wahamiaji kujijenga upya baada ya kurejea nyumbani aliweza kupokea mzigo wa vipodozi na kufungua duka lake na tangu hapo maisha yakamnyookea sasa ameoa na ana familia yake anayoweza kuitunza kupitia biashara ya vipodozi.  

IOM pia ilimsaidia kupata bima ya afya. Anasema hajuti kurejea nyumbani bali kilichosalia ni shukrani,“Nalishukuru sana shirika la IOM kwa sababu kazi za kibinadamu wanazofanya na kusaidia wengine ni kitu kizuri sana kwa maoni yangu” 

Na sasa anawashauri wahamiaji wengine Libya kwamba maji yakizidi unga wasisahau kuwa nyumbani ni nyumbani warejee.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter