Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hadithi ya Sakina: safari yake kuanzia kuwa mjane barubaru hadi kuwa mfanyakazi anayejiamini 

Mwaka 2018 Sakina alikuwa ameajiriwa katika kiwanda cha kutengeneza sabuni huko Kandahar kwa ushirikiano wa IOM.
Photo: IOM Afghanistan
Mwaka 2018 Sakina alikuwa ameajiriwa katika kiwanda cha kutengeneza sabuni huko Kandahar kwa ushirikiano wa IOM.

Hadithi ya Sakina: safari yake kuanzia kuwa mjane barubaru hadi kuwa mfanyakazi anayejiamini 

Wahamiaji na Wakimbizi

Ukosefu wa usawa wa kijinsia huongezeka katika hali za mizozo. Wanawake wameathirika kwa kiasi kikubwa katika suala la usalama wa kibinafsi, upatikanaji wa ajira, rasilimali na huduma za msingi katika mazingira dhaifu, yenye migogoro.  

Wanaathirika sana na umaskini na mchango wao mkubwa wanaoutoa nyumbani huwa hauonekani.  

Katika jamii kama Afghanistan, mila za jadi mara nyingi hufanya iwe vingumu kwa wanawake kupata ajira, kupata mikopo au kuanzisha biashara, ilhali wanawake wakipewa fursa, huwa wanatoa michango muhimu katika ukuaji na maendeleo ya familia zao na jamii zao kwa ujumla. 

Sakina alizaliwa katika kijiji kidogo mkoani Helmand mwaka 1995. Alikuwa na umri wa miaka 5 tu wakati familia yake ilipokimbia Afghanistan mwaka 2000 na kuhamia Pakistan.  

Kwa kuwa aliishi kwa umaskini kwa kiasi kikubwa wakati wa utoto wake, mara nyingi akifanya kazi za nyumbani katika kaya mbalimbali,  

Hata hivyo Sakina alikuwa na ndoto ya kwenda shule kama watoto wa familia alizowahi kuzihudumia. 

Akiwa na umri wa miaka 14, angali bado mtoto anayependa  kucheza na marafiki zake, familia yake ilimjulisha kuwa ataolewa.  

Yeye hakumbuki alivyoitikia uamuzi huo wa wazazi wake. 

"Hata hivyo bado nilikuwa mtoto," Sakina anatabasamu huku akisikitika. 

 

Kazi hii imewezesha Sakina kukidhi mahitaji ya familia ikiwemo kupeleka mwanae shule binafsi.
Photo: IOM Afghanistan
Kazi hii imewezesha Sakina kukidhi mahitaji ya familia ikiwemo kupeleka mwanae shule binafsi.

 Baada ya kuolewa, mambo hayakuwa sawa. Bado alikuwa akiishi kama mkimbizi nchini Pakistan, bila kupata huduma sahihi za msingi.  

Katika umri mdogo wa miaka 19, mumewe aliuawa katika ajali ya barabarani akiwa na ujauzito wa miezi sita.  

Akiwa bado barubaru akaachwa mjane na mama mzazi wa mtoto wa kike. Kufariki ghafla kwa mumewe kulimvunja moyo. Kwa miezi, hakuweza kuacha kulia. 

Licha ya janga lililomsibu ilibidi awe jasiri na kuendelea na maisha ili kumlea binti yake. 

Kuishi Pakistan bila kipato sahihi ilikuwa ngumu sana kwake. Familia ya Sakina iliamua kumrudisha Afghanistan mwaka 2018.  

Aliporudi, alianza kuishi na familia ya shemeji yake. Kwa kuwa hakujua kusoma wala kuandika, pia hakuwa na ujuzi wowote wa kitaalam, alijitahidi kupata chanzo thabiti cha mapato kwa zaidi ya mwaka mmoja.  

Alilazimika kutegemea kazi za mikono ili kumlea binti yake na kulipa kodi ya pango kwa shemeji yake.  

Alifanya kazi za nyumbani katika nyumba tofauti akiosha vyombo na kupika chakula. 

Mwaka 2018, Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM), pamoja na msaada kutoka idara ya wakimbizi na urejeshwaji nchini Afghanistan kwa hiyari iliyoko mjini Kandahar, ilimpa Sakina fursa ya ajira chini ya program ya ujenzi mpya wa maisha na maendeleo nchini Afghanistan (RADA), inaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya (EU).  

Aliajiriwa na kampuni ya sabuni mjini Kandahar ambayo inashirikiana na IOM katika kukuza biashara kwa wakimbizi na wahamiaji.  

Katika kazi yake mpya, alijifunza kutengeneza sabuni na ujuzi mwingine wa kiufundi unaohitajika katika kazi hiyo.  Mwanzoni Sakina alihisi ugumu wa kushirikiana na wenzake kwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye haya. 

 "Mbali na ujuzi wa kiufundi, nimejifunza jinsi ya kushirikiana na watu kutoka asili tofauti na jinsi ya kujadiliana na kuzungumza na wateja. Hizi ndizo stadi ambazo ningehitaji ikiwa ningetaka kuomba kazi bora, ”anasema Sakina anayejiamini Zaidi hivi sasa. 

Kabla ya kazi hii, Sakina alikuwa anashinikizwa sana hadi afya yake ya akili kuathirika.  

Aliogopa kwamba binti yake angekabiliwa na hatima sawa na yeye ikiwa hangeweza kumpa elimu.  

Walakini, baada ya mwaka mmoja katika ajira, wasiwasi wa Sakina umepungua pole pole. Kazi ya kutengeneza sabuni imemsaidia kugharamia familia yake na kumwezesha kumsajili binti yake wa miaka sita katika shule ya kibinafsi mjini Kandahar. 

“Wakati nilikuwa nikifanya kazi za majumbani, nilipata shida ya kujikimu. Mawazo ya kutoweza kumpeleka binti yangu shuleni yalinifanya niwe na wasiwasi sana. Iliathiri afya yangu ya mwili na akili, na sikuweza kuwa na amani, ”anakumbuka Sakina. 

Baada ya kupitia changamoto nyingi kama vile kukosa elimu na kuolewa akiwa mtoto, Sakina ambaye sasa ana umri wa miaka 25 anaelewa kabisa umuhimu wa kuwaelimisha wasichana.  

Anaamini kuwa elimu ndiyo njia pekee ya kujikwamua katika nchi iliyoghubikwa na vita kama Afghanistan. Sakina anatumai kwamba wazazi katika nchi yake wanaipa elimu kipaumbele kwa binti zao na wawaache wawe wanawake wanaofanya kazi, wanaojitegemea kifedha, wenye uwezo wa kufanya maamuzi yao wenyewe, badala ya kuwaoza wakiwa na umri mdogo. 

Hivi sasa anapomzungumzia binti yake, uso wa Sakina unajawa na furaha na matumaini kwa siku zijazo. 

 “Mambo yanabadilika. Wanawake walioelimika sasa wanafanya kazi katika kila nyanja kama vile shule, hospitali, ofisi za serikali na mashirika ya kimataifa. Labda siku moja, binti yangu pia atafanya kazi kwenye shirika la kimataifa, ”anasema Sakina, akiwa na matumaini makubwa.