Hatimaye waethiopia waliokwama Tanzania warejea nyumbani

18 Februari 2020

Baada ya harakati za kuondoka nchini mwao Ethiopia kwenda kusaka maisha ugenini kukwama nchini Tanzania, hatimaye wahamiaji 463 wa taifa hilo la pembe ya Afrika wamerejea nyumbani kufuatia juhudi za pamoja za serikali za Tanzania, Ethiopia na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM.

Wahamiaji  hao wamerejea nyumbani mwezi huu pekee na ndege ya mwisho iliwasili Jumatatu huku wahamiaji wengine wakiwemo Tamrat na Debebe wakitarajiwa kurejeshwa nyumbani katika wiki chache zijazo.

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo Dar es Salaam, Tanzania na Addis Ababa, Ethiopia imemnukuu Tamrat akisema kuwa tangu akiwa mtoto ndoto yake ilikuwa kuwa daktarin au mhandisi.

Hata hivyo kwa kuwa hakuweza kujiunga na Chuo Kikuu aliamua kuhamia na kufanya kazi Afrika Kusini,”  imesema taarifa hiyo.

Yaelezwa kuwa Tamrat aliahidiwa na msafirishaji haramu wa binadamu kuwa atasafiri hadi Kenya kwa basi na kisha atapanda ndege na kusafiri hadi Afrika Kusini ambapo alilipa kati ya dola 3,150 hadi 5,600 kwa safari hiyo.

Hata hivyo ndoto yake ilikoma baada ya lori alimokuwa akisafiria kukamatwa na polisi akinukuliwa akisema kuwa, “usafiri ulikuwa wa machungu kwani  baadhi yao wangalikufa kutokana na kukosa hewa kama tusingalikamatwa na polisi.”

Gari lao lilipokamatwa na polisi walifungwa kwa miaka mitatu  nchini Tanzania.

Debebe, kwa upande wake aliwekwa korokoroni nchini Tanzania kwa miaka minne huku anakumbuka kuwa nyumbani Ethiopia kabla ya kukimbia alikuwa mshona viatu na alilipa dola 4,500 ili kukamilisha safari yake ya Afrika Kusini, ambayo nayo iliishia njiani.

Safari za Tamrat na Debebe za kurejea nyumbani zinafanyika kupitia mpango wa pamoja wa IOM na Muungano wa Ulaya wa kusaidia ulinzi na ujumuishaji wa wakimbizi kwenye pembe ya Afrika na wanasafirishwa kwa ndege ya shirika la ndege la Ethiopia.

IOM inapatia wahamiaji hao misaada kama vile uchunguzi wa kiafya, nguo na viatu kabla ya kuondoka Tanzania na wanapofika Ethiopia wanapatiwa msaada wa matibabu pia, kisaikolojia, na makazi ya muda katika kituo cha mpito cha uhamiaji na hatimaye usafiri wa kuwarejesha kwenye jamii zao.

Tukio la kuondoka kwa wahamiaji hao lilishuhudiwa na Kamishna Mkuu wa huduma za Uhamiaji Tanzania Dkt. Anna Makakala, na Balozi wa Ethipia nchini Tanzania Yonas Yosef Sanbe ambao wamewapatia wahamiaji hao maneno ya usaidizi na matumaini.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter