Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja baada ya makubaliano ya amani, mamilioni ya watoto CAR bado wako hatarini

Jospin (katikati) mkimbizi wa ndani wakiwa kwenye darasa linaloendelshwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, CAR, MINUSCA.
UNICEF/UN0149422/Sokhin
Jospin (katikati) mkimbizi wa ndani wakiwa kwenye darasa linaloendelshwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, CAR, MINUSCA.

Mwaka mmoja baada ya makubaliano ya amani, mamilioni ya watoto CAR bado wako hatarini

Amani na Usalama

Mwaka mmoja tangu kutiwa saini kwa mkataba wa amani kati ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya kati na pande nyingine katika mgogoro, maisha ya mamilioni ya watoto kote nchini bado yanaendelea kutishiwa na vurugu na ukosefu wa chakula, huduma za kiafya, elimu, maji na huduma za kujisafi, imeeleza taarifa iliyotolewa leo na Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF CAR, Christine Muhigana mjini New York Marekani na Bangui, CAR

Bi Muhigana akifafanua zaidi kuhusu hali ilivyo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema, “zaidi ya matukio mabaya 500 ya ukikukwaji wa haki za mtoto yameripotiwa kati ya mwezi Januari na mwezi Desemba mwaka 2019. Yakiwa haya ni matukio yaliyothibitishwa, idadi halisi bila shaka ni kubwa zaidi. Wakati ni vigumu kukadiria ni watoto wangapi wanabaki kuhusishwa na vikosi vyenye kujihami na silaha, watoto hawa ni miongoni mwa waliko hatarini zaidi na hatima yao haiko bayana.”

Lakini pia kuna dalili za matumaini

Mwakilishi huyo wa UNICEF nchini CAR kupitia taarifa hiyo amesema, “tunakaribisha ahadi au kujitolea rasmi kwa makundi zaidi yenye silaha kuzuia ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto na ukweli kwamba watoto wanaendelea kuachiliwa, ama kupitia juhudi za pamoja au kupitia mpango wa kitaifa wa kuwaondoa watoto jeshini.”

Aidha, Bi Muhigana amenukuliwa akisema kuwa wanakaribisha jitihada za nchi kupitisha sheria ya kitaifa ya kulinda watoto. “Wakati sheria hii itakapopitishwa itakuwa chombo muhimu cha kuhakikisha na kutekeleza ulinzi wa watoto wa Afrika ya kati dhidi ya aina zote za ukikukwaji wa haki za msingi ikiwemo kutumikishwa katika makundi yenye sialaha na majeshi.”

Kupitia juhudi za utetezi za UNICEF na wadau wake ikiwemo kampeni ya kuwalinda watoto walioathirika na migogoro iliyozinduliwa mwezi Mei, mswada wa sheria hivi sasa uko mbele ya Bunge ili uweze kuidhinishwa.

“Uanzishwaji wa sheria hii utawakilisha wakati wa kihistoria, na kwa maisha ya watoto leo na kesho.”  Imesisitiza taarifa ya Christine Muhigana.

Aidha ameeleza kuwa pamoja na kwamba kuna hatua kadhaa ambazo zimepigwa kama ufikishaji wa chanjo kwa watoto hata waliko katika sehemu za mbali na usambazaji wa elimu kupitia vipindi vya redio huko Bangui na Bambari, matokeo haya hayatakiwi kuwafanya wabweteke kwani njia ya kuelekea kufanya haki za kila mtoto wa CAR zieleweke vya kutosha na kuheshimika.