Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano ya usitishaji uhasama Libya yako katika jina tu:Salame

Ghassan Salamé wa Lebanon, Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ujumbe wa Msaada wa UN nchini Libya
Eskinder Debebe
Ghassan Salamé wa Lebanon, Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ujumbe wa Msaada wa UN nchini Libya

Makubaliano ya usitishaji uhasama Libya yako katika jina tu:Salame

Amani na Usalama

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNSMIL amesema anasikitika kwamba makubaliano ya Berlin ya usitishaji uhasama nchini Libya yanatekelezwa kwa jina tu na si kwa vitendo.

Ghassan Salame ameyasema hayo leo akitoa tarifa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutokea mjini Brazzaville Congo anakohudhuria mkutano wa Muungano wa afrika AU kuhusu Libya. Bwana Salame amesema “Kufuatia hali inayoendelea hivi sasa nchini Libya nasikitika kusema kwamba muafaka wa amani unatekelezwa kwa jina tu na sio kwa vitendo. Mashambulizi ya makombora yameongezeka sana katika mji mkuu Tripoli katika siku za hivi karibuni, na kuongezeka kwa vifo vya raia kutokana na uvurumishjaji wa makombora usiobagua. Tangu tarehe 6 Januari, tumethibitisha mashambulizi kwa raia 21 kati yao vifo 18 na majeruhi watatu kutokana na matukio yanayohusiana na mapigano ndani na karibu na Tripoli.”

Ameongeza kuwa katika siku mbili zilizopita pekee, watoto wanne wote wakiwa chini ya umri wa miaka 12 wamekufa kwa sababu ya mashambulizi katika makazi eneo la Al Hadhba la Tripoli. Watoto wawili kati ya waliokufa walipoteza maisha katika eneo la shambulio hilo wakati wengine wawili walikufa wakiwa katika uangalizi mkubwa kwenye wodi ya wagonjwa mahituti na wa mwisho alikufa jana alasiri.

Mapigano nje ya Tripoli na ukiukwaji wa mkataba

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema pia wanashuhudia mapiganio makali nje ya mji mkuu Tripoli ambapo tarehe 26 Januari jeshi la serikali ya Libya LNA lilianzisha mashambulizi dhidi ya vikosi vya GNA huko Abu Grain kusini mwa mji wa Misrata na kusababisha mabambano makali yaliyokatili maisha ya makumi ya watu kutoka kila upande.

Tangu Januari 12 mpango wa UNSMIL umeorodhesha vitendo zaidi ya 110 vya ukiukaji wa mkataba wa muafa wa usitishaji uhasama. Salame amesema “Pia ninahofia msaada wa kijeshi unaokuja kwa kila upande. Pande zote kinzani zimeendelea kup[okea kiasi kikubwa cha vifaa, wapiganaji na washauri kutoka wafadhili wa nje, katika hali ambayo inakiuka vikwazo vya silaha lakini pia ahadi iliyotolewa na wawakilishi w anchi hizo mjini Berlin.”

Wapiganaji maluki

Wakati huohuo amesema wapiganaji mamluki wanaosaidia vikosi vya GNA waliletwa mjini Libya kwa ndege kwa maelfu na kusambazwa katika maeneo mbalimbali sambamba na vikosi vya Libya.

Amesema yote haya yanatishia kuzidisha uhasama na kuzua hatari mpya. Wote wanakiuka ari na barua ya mkutano wa Berlin. “Natoa wito kwa pande zote na wafadhili wao kutoka nje kujizuia na vitendo na hatua zozote ambazo zina madhara na badala yake kurejea kwenye ahadi zao za kuhakikisha kuna usitishaji mapigano.

Kuyumba kwa uchumi

Wakimbizi watembea kwenye mwangaza wa jua nje ya Kituo cha UNHCR cha mkutano na safari mjini Tripoli, Libya.
UNHCR/Caroline Gluck
Wakimbizi watembea kwenye mwangaza wa jua nje ya Kituo cha UNHCR cha mkutano na safari mjini Tripoli, Libya.

 

Bwana salame amesema vita nchini Libya pia vinasambaratisha uchumi huku taasisi  na miundombinu vikishindwa kufanya kazi . “deni la kitaifa la Libya hivi sasa limepita bilioni 100 kwa sarafu za nchi hiyo  na linazidi kupanda . Matumizi ya mishahara yamefurutu ada wakati mamlaka ikishindana kuongeza mzigo kwa mishahara hiyo ambayo tayari imelemewa.

Hali ya kibinadamu bado inatia hofu amesema mwakilishi huyo ikiwemo watu kutoweshwa na kuswekwa vizuizini na makundi yenye silaha.” Kuna ripoti za familia kulazimishwa kukimbia nyingine ni kutokana na mahusiano yake na GNA na nyingine ni kutokana na uhusiano wa karibu na utawala uliopita na hatma ya Walibya wengi waliotoweka bado haijulikani.”

Tathimini ya hali halisi 

Bwana. Salame amesisitiza kwamba hali ya kubomoka inafanywa "kwa dharau uhuru wa Libya, haki za msingi za watu wa Libya, na kwa ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya kimataifa na agizo la kimataifa linalozingatia sheria".

Amehitimisha kwa ombi kwa wajumbe wa Baraza la usalama kwamba “kwa  siku zijazo, tafuteni umoja wenu na sauti yenu kukomesha ujinga unaofanyika Libya. Mengi yamo hatarini, pamoja na uaminifu wetu wa pamoja",

UNHCR yasitisha shughuli zake katika (GDF), Tripoli nchini Libya

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limetangaza kuwa kuanzia jana alhamis ya tarehe 30 Januari linasitisha shughuli zake katika kituo cha makutano na kuondoka (GDF), kilichoko mjini Tripoli nchini Libya kutokana na hofu ya usalama na ulinzi wa watu katika kituo hicho, wafanyakazi na wadau baada ya hali ya mgogoro kuwa mbaya mjini Tripoli, Libya.

Mkuu wa UNHCR nchini Libya Jean-Paul Cavalieri amenukuliwa akisema, “kwa bahati mbaya, UNHCR ilibakia na bila chaguo lolote  isipokuwa  kusitisha kazi zake katika GDF mjini Tripoli baada ya kufahamu kuwa mazoezi ya mafunzo, yanayohusisha polisi na jeshi, yanafanyika mita chache kutoka katika makazi ya wasaka hifadhi na wakimbizi.”

UNHCR imesema shughuli zake katika maeneo mengine zinaendelea ispokuwa katika eneo hilo ambalo wanahofia linaweza kulengwa na majeshi.