Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande zote mbili katika mgogoro wa Libya zimekubaliana kuhusu hitaji la kusitisha mapigano- Ghassan Salame

Picha ya juu ya mji mkuu wa Libya, Tripoli, kama ilivyopigwa kutoka kwenye ndege ya UN (Maktaba)
UN/Abel Kavanagh
Picha ya juu ya mji mkuu wa Libya, Tripoli, kama ilivyopigwa kutoka kwenye ndege ya UN (Maktaba)

Pande zote mbili katika mgogoro wa Libya zimekubaliana kuhusu hitaji la kusitisha mapigano- Ghassan Salame

Amani na Usalama

Msuluhishi wa Umoja wa Mataifa anayeongoza mazungumzo mjini Geneva Uswisi ili kusitisha mapigano nchini Libya amesema hii leo kuwa maofisa wa ngazi za juu kutoka pande zote mbili za mgogoro wamekubaliana kuhusu hitaji la usitishwaji mapigano wa kudumu uchukue nafasi ya hali ya kutokuwa na uhakika iliyopo hivi sasa.

Msuluhishi huyo ambaye pia ni Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL Bwana Ghassan Salame amesema, “mazungumzo haya yanalenga kusikiliza kwa makini msimamo wa pande zote mbili kuhusu masharti yao ya kupokea mabadiliko haya ya kutoka kutokuwa na uhakika hadi kuwa na usitishaji mapigano wa kudumu.”

Pande hizo mbili zinazofahamika kama 5+5 Kamisheni ya pamoja ya kijeshi ya Libya, wanakutana baada ya miezi mitano ya mgogoro katika viunga vya mji wa Tripoli na serikali ya mkataba wa kitaifa, GNA na jeshi lililojitangaza lenyewe la Libyan National Army, LNA linaloongozwa na kamanda Khalifa Haftar ambao walizingira mji mkuu mnamo mwezi Aprili mwaka jana.

Hata hivyo Bwana Salame ameonya kuwa uwezekano wa hali ya usalama kudorora zaidi bado upo pamoja na wito wa usitishashi mapigano uliotolewa mapema mwezi Januari na Rais wa Urusi Vladmir Putin na wa Uturuki Tayyip Erdorgan.

Vikwazo vya ununuzi wa silaha vimekiukwaa mara kwa mara

Ingawa makubaliano ya kusitisha mapigano yamekubaliwa na pande zote mbili, Bwana Salame amesema wakati huo huo, vikwazo vya kimataifa vya ununuzi wa silaha vimekiukwa mara kwa mara tangu mwaka 2011, huku kukiwa na ushahidi wa ongezeko la msaaada kutoka nje.

“Tuna ushahidi mpya wa vifaa vipya lakini pia wapiganaji wapya-wapiganaji ambao siyo watu wa Libya, ambao wanajiunga na kambi hizi mbili. Kwa hivyo, tunaamini kuwa vikwazo vya silaha vinakiukwa na pande zote mbili.” Amesisitiza Bwana Salame.

Akieleza changamoto za kufikia matokeo chanya katika mazungumzo ya Geneva Bwana Salame amekuwa muwazi kwa kusema, “hii ni mara ya kwanza, kwa muda mrefu, maofisa wa ngazi ya juu wa pande zote mbili, kimsingi, ni mara ya kwanza kabisa. Kwa hivyo msitegemee kutoka katika mkutano mmoja wa jana mchana, kutatua masuala yote.”