Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nina imani na Baraza la Usalama katika kusongesha mchakato wa amani ya kudumu Libya- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres(kushoto) akizungumza na wanahabari kuhusu hali ya Libya baada ya kuhutubia kwenye mkutano wa mashauriano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Januari 21, 2020.
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres(kushoto) akizungumza na wanahabari kuhusu hali ya Libya baada ya kuhutubia kwenye mkutano wa mashauriano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Januari 21, 2020.

Nina imani na Baraza la Usalama katika kusongesha mchakato wa amani ya kudumu Libya- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja huo jijini New York, Marekani na kuelezea matumaini yake kwa Baraza la Usalama la chombo hicho katika kusongesha makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni huko Berlin, Ujerumani kuhusu mzozo unaoendelea nchini Libya.

Guterres amezungumza na wanahabari hao baada ya kupatia muhtasari wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kile kilichotokea Berlin ikiwemo taarifa ya pamoja yenye lengo la kupatia suluhu mzozo wa Libya.

Amesema ingawa pande mbili kwenye mzozo huo ambazo ni serikali ya makubaliano ya kitaifa, GNA na vikosi wafuasi wa Jenerali Khalifa Haftar walikuwepo Berlin lakini hawakukutana,  "lakini ilikuwa mara ya kwanza kuweza kuketi kwenye meza moja nchi zote ambazo zina ushawishi wa moja kwa moja au wa njia nyingine kwenye mzozo huo na kuweza kuzishawishi nchi hizo zisiingilie na ziahidi kuunga mkono sitisho la mapigano, kuweka vikwazo vya silaha na kuona zinaahidi kuunga mkono mchakato wa kisiasa, na kuepuka ukiukwaji wa haki za kibinadamu za kimataifa na kuunga mkono taasisi za kiuchumi na kiusalama na hilo lilikuwa muhimu sana."

Lakini Bwana Guterres amesema “hata hivyo bado safari ni ndefu kwa kuwa ingawa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda fulani yapo,  bado kuna maeneo  yanakiukwa kwa hiyo tunachotaka sasa ni kuwepo na sitisho kabisa la mapigano na hatimaye makubaliano ya kisiasa. Na sisi tunaamini kuwa nchi zenye ushawishi na pande zote kinzani nchini Libya zinaweza kusaidia kufanikisha hilo."

Alipoulizwa iwapo ana imani na Baraza la Usalama katika kufanikisha amani Libya, Katibu Mkuu amesema kuwa “bila shaka kwa kuwa nchi tano zenye uanachama wa kudumu wa baraza hilo zilikuwepo Berlini na zilikubaliana na tamko la pamoja lililotolewa mwishoni mwa mkutano, kwa hiyo nina imani kubwa.”

Bwana Guterres amesema kuwa ni kwa ushawishi huo huo ana imani kuwa pande hizo zitakutana Jumanne ijayo ili kusongesha harakati za kuleta amani ya kudumu nchini Libya.

Mkutano wa kimataifa kuhusu Libya ulifanyika tarehe 19 mwezi huu huko Berlin nchini Ujerumani na ulileta pamoja wakuu mbalimbali wa nchi na serikali, mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika, Katibu Mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu, marais wa Jumuiya ya Muungano wa Ulaya na tume ya Muungano wa Ulaya na wadau muhimu wa Libya ni wa kusaidia juhudi za kukomesha vita nchini Libya.