Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rudisheni mamlaka ya Myanmar kwa serikali iliyochaguliwa-Baraza la haki za binadamu. 

Yangon, Myanmar.
UN News/Nyi Teza
Yangon, Myanmar.

Rudisheni mamlaka ya Myanmar kwa serikali iliyochaguliwa-Baraza la haki za binadamu. 

Haki za binadamu

Kitendo cha jeshi kuchukua mamlaka kwa nguvu ni hatua kubwa kurudi nyuma kwa Myanmar, ambayo imekuwa katika njia ya kidemokrasia kwa miaka kumi iliyopita, amesema Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Nada An-Nashif wakati wa kikao cha Baraza na haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.  

Washiriki wa mkutano wamepitisha azimio ambalo wanadai kuresjeshwa kwa udhibiti chini ya serikali  

Wakirejelea tukio la Februari mosi, jeshi la Myanmar lilimshikilia Kiongozi mkuu Aung San Suu Kyi na viongozi wengine, wakiwashutumu kwa "wizi wa uchaguzi" mnamo Novemba 2020. Kamanda wa Jeshi Min Aung Hlaing hadi sasa ametangaza hali ya hatari kwa mwaka mmoja, hadi uchaguzi ujao. Tangu kunyakuliwa kwa madaraka, maandamano yameendelea kote Myanmar, huku vikosi vya usalama vikiripotiwa kutumia silaha kali kuwatawanya. 

Katika hotuba yake, Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Nada Al-Nashif ametaka kuachiliwa mara moja kutoka gerezani kwa "uongozi uliochaguliwa kidemokrasia wa Myanmar", pamoja na mamia ya wanaharakati, waandishi wa habari na wawakilishi wa asasi za kiraia walioshikiliwa wakati wa maandamano hayo. Amewataka wanajeshi kuheshimu matakwa ya watu wa Myanmar ambao walipiga kura katika uchaguzi wa Novemba na kurudisha udhibiti wa nchi hiyo kwa serikali ya raia iliyochaguliwa kisheria. 

"Wanajeshi wa Myanmar wameonesha tena kupuuza sheria na kusadiki kwamba wako juu ya sheria," amesema Mjumbe Maalum kuhusu Myanmar, Tom Andrews, akizungumza kwenye kikao hicho. Wajumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa, wanateuliwa na Baraza la Haki za Binadamu, lakini sio wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa. 

Kwa mjibu wa mtaalam huyo wa kujitegemea, hata ikiwa ukiukaji fulani ulifanywa wakati wa uchaguzi wa Novemba, hii sio sababu ya kutangaza hali ya hatari, kukamata uongozi wa nchi na "kujaribu kutokomeza demokrasia." Bwana Andrews amesema huku akiwataka wajumbe wa Baraza kuwaunga mkono waandamanaji.  

Mwakilishi wa Myanmar akihutubia mkutano huo amesema, wanajeshi walianzisha udhibiti nchini humo kwa mujibu wa Katiba, kutokana na udanganyifu wa uchaguzi. Amesema kuwa Baraza la Utawala la Jimbo liliundwa mnamo Februari 2, na kubainisha kuwa ni pamoja na wanajeshi 8 na raia 8. Wakati huo huo, mwakilishi wa Myanmar ametoa wito kwa jamii ya kimataifa "kushughulikia hali hiyo ngumu kwa uelewa" na kuunga mkono nchi yake. 

Wazungumzaji wengi wamelaani  vikali utekaji nyara uliofanywa na jeshi na wakajiunga na wito wa kuachiliwa kwa waliokamatwa, lakini msimamo mwingine ukatolewa na China ambao wamesema kilichotokea ni "mambo ya ndani ya Myanmar" na ikataka kuheshimiwa "uhuru wa nchi hii." 

Urusi nayo imesema mwendo wa majadiliano katika Baraza la Haki za Binadamu,"tunalazimika kusema kuwa majadiliano kuhusu hali ya Myanmar katika Baraza la haki za binadamu yanafanyika kwa njia ya kisiasa na haiwezi kuchangia katika kuboresha hali ya haki za binadamu. katika nchi hii.” Mwakilishi wa Shirikisho la Urusi Dmitry Vorobiev amesema. 

Mwisho wa kikao hicho maalum, washiriki wake kwa makubaliano wamepitisha azimio ambalo linahitaji kurudishwa kwa nguvu ya uongozi wa nchi uliochaguliwa, kuachiliwa kwa haraka na bila masharti kwa raia wote waliowekwa kizuizini kinyume cha sheria, pamoja na kiongozi Aung San Suu Kyi na viongozi wengine, na vile vile kuondoa vizuizi kwenye mawasiliano na upatikanaji wa mitandao ya kijamii, vizuizi ambavyo vimewekwa na jeshi. Urusi imesema kuwa "inajitenga na makubaliano juu ya azimio hili." 

TAGS: Myanmar, Aung San Suu Kyi, Baraza la haki za binadamu.