Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vituo vya wakimbizi vyazidiwa Uganda maelfu wakiendelea kumiminika toka DRC:UNHCR

Wakimbizi wapya kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wakiwasili kwenye kituo cha  muda cha mapokezi huko Sebagoro, wilaya ya Hoima nchini Uganda
UNHCR/Michele Sibiloni
Wakimbizi wapya kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wakiwasili kwenye kituo cha muda cha mapokezi huko Sebagoro, wilaya ya Hoima nchini Uganda

Vituo vya wakimbizi vyazidiwa Uganda maelfu wakiendelea kumiminika toka DRC:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Mapigano mapya Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC yamewafurusha watu takribani 7500 na kuwalazimisha kukimbilia nchi jirani ya Uganda tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Juni na kuongeza shinikizo katika vituo vya wakimbizi ambavyo tayari vilikuwa vimezidiwa uwezo limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswis kuhusu hali hiyo hii leo, msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic amesema mapigano mapya baina ya makundi kinzani ya Hema na Lendu ymewalazimisha watu wapatao 311 kuingia Uganda kila siku , ikiwa ni mara mbili ya idadi ya wakimbizi waliokuwa wakiwasili Uganda mwezi Mei ambao walikuwa 145 kwa siku. Na kuongeza kwamba wanaowasili wanasimulia ukatili wa hali ya juu

SAUTI YA ANDREJ MAHECIC

“Makundi yenye silaha yameelezwa kushambulia vijiji , kuchoma moto na kupora nyumba na kuua wanaume, wanawake na Watoto Wengi wanakimbilia Uganda kupitia Ziwa albert wakitokea jimbo la Ituri ambako watu waliotawanywa tangu mapema mwezi Juni sasa wanakadiriwa kuwa 300,000.”

Ameongeza kuwa watu wanawasili na vifurushi vyao wakihifia kwamba hawatoweza kurejea nyumbani hivi karibuni. Na kwa wengine waliokimbnia hatari ya kifo hawana chochote Zaidi ya nguo, huku ltakriban theluthi mbili ya watu hao ni Watoto walio chini ya umri wa miaka 18. Mahecic ameongeza kwamba

SAUTI YA ANDREJ MAHECIC 

“Wakimbizi wanatuambia kwamba watu Zaidi huenda wakawasili Uganda hivi karibuni . Hata hivyo baadhi wameripotiwa kuzuiliwa kuondoka DRC na makundi yenye silaha , huku wengine wakihaha kumudu nauli ya safari ya boti ambayo ni swwa na chini ya dola 6.

Uganda kwenyewe kwa mujibu wa UNHCR vituo vya muda mpkanani na vya mapokezi vimezidiwa uwezo na wakimbizi wapya wanaowasili wanapelekwa kwanza kwenye kituo cha Sebagoro kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya na kisha kupelekwa kwenye kituo cha Kagoma kituo ambacho kwa sasa kina wakimbizi wapya 4600 ikiwa ni wakimbizi 1,600 zaidi ya uwezo wake.

UNHCR inaiomba jumuiya ya kimataifa kuongeza ufadhili  kwani hadi sasa Uganda imepokea dola milioni 150 tu kwa ajili ya wakimbizi ikiwa ni asilimia 17 pekee ya ombi la dola milioni 927 zinazohitajika.

TAGS: Hema, Lendu, DRC. Uganda, wakimbizi