Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la mauaji na unyanyasaji mwingine dhidi ya binadamu mashariki mwa DRC linatisha-UNHCR

Machafuko katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC yansababisha watu kukimbilia nchi jirani.
UNICEF/Madjiangar
Machafuko katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC yansababisha watu kukimbilia nchi jirani.

Ongezeko la mauaji na unyanyasaji mwingine dhidi ya binadamu mashariki mwa DRC linatisha-UNHCR

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, hii leo mjini Geneva Uswisi limeeleza kuwa linashitushwa na ongezeko la vurugu zinazotekelezwa dhidi ya raia katika jimbo la Ituri na Kivu Kaskazini, majimbo mawili yaliyoko katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya kidemkrasia ya Congo, DRC, kutokana na shughuli za makundi yenye silaha na pia uwezo mdogo wa vikosi vya usalama kukomesha vurugu.

UNHCR kupitia msemaji wake, imesema katika miezi ya hivi karibuni, matukio haya yamesababisha ongezeko la ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, makumi ya nyumba zimechomwa moto na maelfu ya watu kutawanywa.

Imeelezwa kuwa machafuko hayo katika majimbo hayo mawili hayana uhusiano lakini yanashabihiana. Makundi yenye kujihami kwa silaha, mengi yakiwa yanatumia msingi wa ukabila na wakati mwingine kwa kushirikiana na makundi mengine, hushambulia jamii kwa lengo la kutaka kujiongezea udhibiti wa ardhi na rasilimali.

Mathalani hivi karibuni, jumanne ya tarehe 17 mwezi huu wa Septemba, raia 14 waliuawa kinyama na wanne walijeruhiwa katika eneo la Bukatsele jimbo la Ituri. Waliopoteza maisha ni pamoja na watoto 11 wenye umri kati ya miezi saba na miaka 15, ambao wote waliuawa kwa kupigwa risasi na kisha kukatwa viungo. Mashambulizi haya yanayoilenga jamii ya Hema, yanaaminika kuwa yameandaliwa na kundi lililojihami na silaha la watu wa jamii ya Lendu. Siku uliyofuata, raia wengine 12, watatu wanawake na watoto wanne, waliuawa katika maeneo matatu tofauti ikiwemo kambi inayowahifadhi wakimbizi wa ndani. Waathirika wote walikuwa watu wa jamii ya Hema.

Aidha msemaji wa UNHCR amefafanua kuwa, mauaji haya ni moja tu ya mauaji ya hivi karibuni katika mlolongo wa mauaji kwenye maeneo ya Djugu na Mahagi jimboni Ituri. Kwa mujibu wa takwimbu zilizokusanywa na ofisi ya haki za binadamu nchini DRC tangu tarehe mosi ya mwezi Juni, takribani raia 197 wameuawa jimboni Ituri katika mashambulizi yanayoaminika kutekelezwa na wapiganaji wa Lendu. Waathirika wote ni watu wa jamii ya Hema au Alur. Idadi hii haikujumuisha mauaji ya wiki iliyopita.

UNHCR imesema pia kuwa katika kipindi hicho hicho cha Juni mosi, takribani waathirika 51 wa ubakaji na aaina nyingine za unyanyasaji wa kingono uliripotiwa jimboni Ituri. Wengi wakiwa wamebakwa na makundi makubwa ya watu.

Kwa mujibu wa ripoti, wakati wa operesheni za kijeshi dhidi ya wapiganaji wa Lendu, vikosi vya usalama viliwaua takribani raia 17 katika kile kinachoongeza mauaji ya raia katika matukio ya kulipiza kiasi dhidi ya makundi yenye silaha.

“Hili ni suala lenye umuhimu mkubwa.” Imesema UNHCR.

Aidha UNHCR imesema kuwa hali Kivu kusini pia inatia wasiwasi kutokana na uwepo wa makundi yenye silaha yanayohusishwa na jamii kadhaa kupigana na kutekeleza mashambulizi dhidi ya raia. Katika kipindi cha siku sita, kuanzia tarehe 8 hadi 14 mwezi huu wa Septemba, takribani raia wanane waliauawa katika jimbo hilo la Kivu Kusini.

Wimbi la vurugu limesababisha watu wengi kukosa makazi na kwa mujibu wa OCHA, takribani watu 230,000 wamefurushwa na kupoteza makazi katika Ituri tangu mwezi Juni na wengine 20,500 katika Kivu Kaskazini. Wengi wao hivi sasa wanaishi katika hali mbaya ya isiyo ya kibinadamu.

“Katika eneo la Ituri, kuna mtindo mpya unaoleta wasiwasi mkubwa katika wiki za hivi karibuni kutokana na kuongezeka kwa matendo ya unyanyasaji ambapo wapiganaji wanawalenga watu waliotawanywa kwa kukosa makazi.” Imesema taarifa ya UNHCR.

UNHCR imesema inakaribisha ahadi ya rais wa DRC, Félix Tshisekedi ya kuboresha hali ya haki za binadamu mashariki mwa nchi yake na pia hatua yake ya kutaka kufanya mazungumzo na waasi. Aidha shirika hilo la kuhudumia wakimbizi limezitaka mamlaka kutatua vyanzo vinavyosababisha vurugu na mapigano kati ya jamii na jamii.