Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afya bora si haki ya matajiri pekee, bali kila mtu- UNAIDS

Dawa za kupunguza makali ya VVU , ARV's zimeokoa maisha ya watu wengi duniani kote.
UN
Dawa za kupunguza makali ya VVU , ARV's zimeokoa maisha ya watu wengi duniani kote.

Afya bora si haki ya matajiri pekee, bali kila mtu- UNAIDS

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kutokomeza Ukimwi, UNAIDS linatoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa haki ya afya kwa wote inazingatiwa kwa kupatia  kipaumbele uwekezaji wa umma katika sekta ya afya.

Wito huo wa UNAIDS unakuja wakati huu ambapo takribani nusu ya wakazi wa dunia hawana uwezo wa kupata huduma muhimu za afya, ambapo katika kila dakika mbili mwanamke mmoja anafariki dunia wakati akijifungua.

UNAIDS inasema walio katika hali ngumu zaidi ya kupata huduma muhimu za afya ni wale wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, VVU, wanaume mashoga, makahaba, wanaojidunga madawa ya kulevya, watu waliobadili jinsi zao, wahamiaji, wakimbizi na hohehahe.

Ni kwa mantiki hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima kupitia taarifa ya shirika lake iliyotolewa leo Davos na Geneva, Uswisi anasema kuwa, haki ya afya inawaepuka maskini na watu wanaojikwamua kutoka kwenye umaskini wanazidi kukandamizwa kutokana na gharama kubwa zisizokubalika za huduma za afya.

Amesema wakati maskini wanahaha kusaka huduma, asilimia 1 ya watu matajiri zaidi duniani  wananufaika na teknolojia za kisasa zaidi za sayansi ya tiba.

Akichambua takwimu, Bi. Byanyima amesema takribani watu milioni 100 wanatumbukia kwenye lindi la umaskini kwa sababu wanalazimika kugharimia huduma za afya na zaidi ya watu milioni 930 wanatumia asilimia 10 ya kipato chao cha kaya kugharimia huduma za afya,

Mandisa Dukashe na familia yake ni wakazi wa Eastern Cape, Afrika Kusini. Mandisa ni muuguzi na anahusika na udhibiti wa VVU na yeye mwenyewe anaishi na VVU. Lakini mumewe na binti zake wamepima VVU na hawana virusi hivyo.
AFP PHOTO/MUJAHID SAFODIEN
Mandisa Dukashe na familia yake ni wakazi wa Eastern Cape, Afrika Kusini. Mandisa ni muuguzi na anahusika na udhibiti wa VVU na yeye mwenyewe anaishi na VVU. Lakini mumewe na binti zake wamepima VVU na hawana virusi hivyo.

“Katika mataifa mengi, watu wananyimwa haki ya afya au wanapata huduma duni ya afya kwa sababu ya gharama kubwa wazisoweza kukidhi. Unyanyapaa na ubaguzi unawanyima watu maskini na walio hatarini, hususan wanawake haki yao ya afya,”  amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNAIDS.

Kama hiyo haitoshi, kila wiki vijana wa kike 6000 wanaambukizwa VVU na katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, barurabu 5 kati ya 4 wanaoambukizwa VVU ni wasichana.

UNAIDS inasema licha ya mafanikio makubwa katika kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI bado kulikuwepo na maambukizi mapya milioni 1.7 ya VVU mwaka 2018 huku watu milioni 15 wanasubiri kupata tiba ya kupunguza makali ya VVU.

Bi. Byanyima amesema jawabu ni uwekezajiwa umma katika sekta ya afya kwa kuwa, “pindi bajeti ya afya inapopunguzwa au inapokuwa haitoshelezi, ni watu maskini au watu walio pembezoni ndio hususan wanawake na wasichana ndio wanaopoteza haki yao ya afya na wanabeba mzigo wa kuhudumia familia zao.”

Amesema kuwa huduma ya afya kwa wote ni chaguo la kisiasa ambalo serikali nyingi hazichagui.

Mathalani ametoa mfano wa Thailand akisema licha ya kipato kidogo imepunguza idadi ya vifo vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano kutoka hadi watoto 9 kati ya watoto 1000 ilhali Marekani nchi tajiri ni kiwango ni watoto 6 kati ya 1000.

“Mafanikio ya Thailand yametokana na uwekezaji wa umma katika sekta ya afya ambao unampatia kila raia huduma za msingi katika kipindi chote cha uhai wake,”  amesema Bi. Byanyima ambaye yupo Davos akishiriki jukwaa la kiuchumi duniani la mwaka 2020.

Bi. Byanyima anatumia mkutano huo kusihi serikali kutekeleza ahadi zao za kufanikisha huduma ya afya kwa wote ili asiwepo mtu yeyote anayeachwa nyuma katika kufanikisha ahadi hiyo iliyoazimiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka jana wa 2019 jijini New York, Marekani.