Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa dawa mpya za viuavijasumu unatishia juhudi za kupambana na usugu wa dawa hizo:WHO

Mchoro wa mfano wa bakteria sugu ya kifua kikuu ya Mycobacterium.
CDC/Alissa Eckert, James Archer
Mchoro wa mfano wa bakteria sugu ya kifua kikuu ya Mycobacterium.

Ukosefu wa dawa mpya za viuavijasumu unatishia juhudi za kupambana na usugu wa dawa hizo:WHO

Afya

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la afya duniani WHO inasema ukosefu wa dawa mpya za viuavijasumu au antibiotics ni tishio kubwa la juhudi za kimataifa za kupambana na usugu wa dawa hizo na hivyo kuweka hatarini Maisha ya mamilioni ya watu

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya WHO sababu kubwa ya ukosefu wa dawa hizo mpya ni kushuka kwa uwekezaji binafsi na kukosekana na ubunifu katika kutengeneza dawa mpya za viuavijasumu.

Ripoti mbili zilizotolewa kwa pamoja zote zinadhihirisha udhaifu wa kwa mawakala wa dawa za viuavijasumu.

Zimefafanua kwamba katika dawa aina 60 zilizo katika mchakato wa kutengenezwa hivi sasa 50 zikiwa ni za viuavijasumu na 10 za kibaolojia zinaleta faida ndogo sana katika kutibu na chache tu ndizo zinzoweza kupambana na bakteria sugu, na zile zilizoko katika majaribio ambazo ndio za kibunifu zaidi zitachukua miaka kabla ya kuwafikia wagonjwa.

Akifafanua zaidi kuhusu usugu wa dawa hizo na tishio lililopo Dkt. Peter Bayer  mshauri wa ngazi ya juu wa WHO kuhusu dawa za viuavijasumu amesema

(SAUTI YA DKT PETER BAYER)

“Usugu wa dawa maanake ni kwamba bakteria wanazidi kuwa sugu dhidi ya dawa za viuavijasumu zilizopo, ni moja ya tishio kubwa la afya , kuna watu 33,000 wanakufa kila mwaka Ulaya kutokana na maambukizi yaliyokuwa sugu kwa dawa, Marekani tawkimu za karibuni zinakadiria kwamba kuna maambukizi milioni 2.8 ambayo ni ya bakteria sugu, hivyo ni tatizo kubwa na tunajua linaweza kuathiri kila mtu hivyo kuwa na dawa za viuavijasumu zinazofanya kazi ni muhimu. Tatizo hili linasambaa na tunaupungufu wa dawa za viuavijasumu ambazo zinafanyakazi kukabiliana na bakteria hawa sugu”

Naye mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedross Adhamon Ghebreyesus akisistiza hali halisi amesema “ Hakujawahi kuwa na tishio kubwa na la dharura kama la sasa ambalo linahitaji suluhu ya haraka. Mikakati mingi inafanyika kupunguza usugu wa dawa lakini pia tunahitaji nchi na viwanda vya madawa kuchukua hatua na kuingilia kati na kuchangia kwa ufadhili endelevu na dawa mpya bunifu.”

Ripoti hizo pia zimebaini kwamba utafiti na maendeleo kwa ajili ya dawa za viuavijasumu unaendeshwa na makampuni madogo au ya wastani na makampuni makubwa ya madawa yanaendelea kuondoka katika sekta hiyo.

Ripoti hizo pia zimeonya kwamba matibabu mapay pekee hayatoshi kupambana na tishio la usugu wa dawa za viuavijasumu, hivyo WHO inashirikiana na nchi wanachama na wadau wengine kuboresha uzuiaji wa maambukizi na kudhibiti na kuhakikisha matumizi sahihi ya dawa zilizopo na zijazo.