Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utengenezaji wa dawa za kuua vimelea au viuavijasumu umedorora- WHO

Mtoto Kadia alizaliwa akiwa ameambukizwa ugonjwa ambao ni hatari kwa watoto wachanga. Hata hivyo nafuu yake ni kwamba aliweza kupata dawa ya viuavijasumu punde tu baada ya kuzaliwa la sivyo angalifariki dunia. Pichani akipatiwa dawa na muuguzi nchini Mali
© UNICEF/UN0188875/Njiokiktjien
Mtoto Kadia alizaliwa akiwa ameambukizwa ugonjwa ambao ni hatari kwa watoto wachanga. Hata hivyo nafuu yake ni kwamba aliweza kupata dawa ya viuavijasumu punde tu baada ya kuzaliwa la sivyo angalifariki dunia. Pichani akipatiwa dawa na muuguzi nchini Mali

Utengenezaji wa dawa za kuua vimelea au viuavijasumu umedorora- WHO

Afya

Kasi ya kutengeneza  aina mpya ya dawa za kuua vimelea au bakteria ni ndogo  mno kiasi kwamba haitoshelezi kukabiliana na ongezeko la usugu wa dawa hizo zijulikanazo pia kama viuavijasumu.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, iliyotolewa leo Geneva, Uswisi inanukuu ripoti yam waka 2021 inayosema kuwa “uendelezaji wa aina mpya ya viuavijasumu sambamba na majaribioi ya dawa mpya vimedorora kiasi kwamba havikidhi mahitaji ya dunia.”

Hali halisi ya uzalishaji

Tangu mwaka 2017 ni aina 12 tu za dawa za kuua vimelea au viuavijasumu ndio zimeidhinishwa, ambapo 10 kati ya hizo ni zinafanana na mfumo ulioko wa dawa sugu za kuua vijiumbe maradhi, au AMR.

“Kuna pango  kati ya ugunduzi wa tiba mpya za viuavijasumu na zaidi ya yote ubunifu wa matibabu,” amesema Dkt. Hanah Balkhy, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa WHO akihusika na AMR.

Amesema hali hiyo inazusha changamoto kubwa katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa yanayohitaji viuavijasumu na hivyo kumweka kila mkazi wa dunia katika hatari ya maambukizi ya vimelea ikiwemo magonjwa ya kawaida kabisa.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa mwaka wa WHO, mwaka 2021 kulikuweko na aina mpya 27 za dawa aina ya viuavijasumu kwa ajili ya majaribio ikiwa ni pungufu ikilinganishwa na 31 mwaka 2017.

Nini kikwazo?

WHO inataja vikwazo vya kuibuka na dawa mpya kuwa ni pamoj ana mlolongo mrefu wa uthibitishwaji wa dawa, gharama kubwa za utengenezaji na fursa finyu ya dawa kuidhinishwa.

“Inachukua kati ya miaka 10 hadi 15 kwa dawa aina ya viuavijasumu kuingia kwenye hatua za awali hadi kufikishwa kwenye majaribio,” imesema taarifa hiyo ya WHO.

Janga la COVID-19 nalo pia limekwamisha majaribio ya dawa.

Hata hivyo WHO limetoa wito kwa serikali na sekta binafsi kuwekeza katika tafiti na uendelezaji wa dawa hasa zile zinazoweza kuwa na athari chanya kwenye maeneo yenye rasilimali kidogo, ambako huko ndio kuna usugu zaidi wa dawa aina ya viuavijasumu.