Hakuna muda wa kusubiri, usugu wa dawa ni janga- Ripoti

29 Aprili 2019

Jopo lililoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na wadau kubonga bongo kuhusu mbinu bora na endelevu za kukabiliana na usugu wa viuavijiumbe maradhi au antimicrobial limetoa ripoti yake yenye mapendekezo makuu manne kwa lengo la kuondokana na tatizo hilo.

Likiwa limefanya vikao kuanzia  mwezi Machi mwaka 2017 kufuatia azimio la kisiasa lililopitishwa na viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2016, jopo hilo la watu 30 limesema hakuna wakati wa kusubiri na kwamba iwapo dunia haichukui hatua za dharura usugu wa viuavijiumbe maradhi utakuwa ni janga katika vizazi na vizazi.

Ripoti yake iliyotolewa leo ikipatiwa jina Hakuna Muda Wa Kusubiri:Kulinda Mustakabali Dhidi Ya Usugu Wa Viuavijiumbe Maradhi imeongeza kuwa usugu wa dawa hizo ni janga la dunia na unatishia maendeleo ya karne kwenye sekta ya afya na pia kufanikiwa kwa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Kwa mantiki hiyo, ripoti inasema kwa kuwa vichocheo vya usugu wa dawa hizo vinapatikana kwa binadamu, wanyama, mimea, vyakula na mazingira hatua moja na endelevu ya kiafya  ni muhimu ili kuleta wadau kwa dira na malengo ya pamoja.

Usugu wa dawa za kuua vijiumbe unazuia uzuiaji na matibabu ya maambukizi yanayosababishwa na ikiwemo viini.
Picha: WHO
Usugu wa dawa za kuua vijiumbe unazuia uzuiaji na matibabu ya maambukizi yanayosababishwa na ikiwemo viini.

Ripoti hiyo yenye kurasa 28 imetoa mapendekezo manne kufanikisha hilo ambapo mosi inataka kuchagiza maendeleo ndani ya mataifa mathalani kwa kuweka mifumo endelevu ya kitaifa ya kupunguza maambukizi katika ngazi mbalimbali za kijamii na kuwepo kwa watoa huduma wa afya wenye ujuzi wa kupatia wagonjwa viua vijasumu.

Pili inataka ubunifu na hivyo fedha zaidi katika utafiti na uendelezaji wa aina mpya za chanjo, viuavijiumbe maradhi na mbinu salama za kutupa takasumu za kitabibu.

Ripoti pia inapendekeza ushirikiano wa kimataifa kwa hatua bora zaidi pamoja na uwekezaji zaidi kupitia misaada rasmi ya maendeleo na ushirikiano wa nchi za kusini kwa hatua endelevu dhidi ya usugu wa viuavijiumbe maradhi.

Jopo lililokuwa na wenyeviti wenza, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus lilitambua kuwa viuavijiumbe maradhi ni dawa muhimu katika kukabili magonjwa kwa binadamu na viumbe vya majini na ardhini lakini matumizi yasiyo sahihi yamesababisha usugu wa dawa hizo.

Ripoti hiyo itawasilishwa wakati wa mkutano wa sasa wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter