Mwaka 2020 ni mwaka wa afya ya mimea ambayo mara nyingi hupuuzwa-UNEP/FAO

Zao la kokoa
©UNDP Ecuador
Zao la kokoa

Mwaka 2020 ni mwaka wa afya ya mimea ambayo mara nyingi hupuuzwa-UNEP/FAO

Tabianchi na mazingira

Mashirika ya Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira duniani UNEP, na la chakula na kilimo FAO yamesema mimea ndio kila kitu katika kuhakikisha uhai wa mamilioni ya watu duniani na sayari tunayoishi, lakini cha kusikitisha ni kwamba mara nyingi mimea hiyo haipewi uzito unaostahili.

Kwa mujibu wa tarifa iliyotolewa na mashirika hayo “mwaka 2020 umetengwa kuwa mwaka wa afya ya mimea” kwa kutambua mchango na thamani ya mimea hivyo kwa maisha ya viumbe duniani.

 

Shirika la mazingira UNEP linasema mimea ni chanzo kikubwa cha hewa tuvutayo na asilimia kubwa ya chakula tunachokula, lakini changamoto imekuwa ni kupuuza kuhakikisha mimea hiyo iko katika afya bora na kuweza kuzalisha zaidi.

Na hii shirika la FAO linasema inaweza  kuwa na athari mbaya sana, likikadiria kwamba hadi asilimia 40 ya mimea ya chakula hupotea kila mwaka kutokana na magonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea.

Limeongeza kuwa hali hii imewaacha mamilioni ya watu duniani bila chakula cha kutosha na kusababisha athari kubwa katika kilimo ambacho ndio uti wa mgongo na chanzo kikuu cha kipato kwa familia masikini vijijini.

Na kwa sababu hizo UNEP na FAO wanasema ndio maana Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliamua kuutangaza mwaka 2020 kuwa mwaka wa afya ya mimea.

Akisistiza umuhimu wa afya ya mimea mtaalam wa UNEP Marietta Sakalian amesema “ Afya ya mimea zaidi na zaidi iko katika tishio. Mabadiliko ya tabianchi na shughuli za binadamu vimemomonyoa mfumo wa maisha, kupunguza bayoanuai na kuweka mazingira mapya ambayo watutu wanashamiri.”

Ameongeza kuwa wakati huohuo safari za kimataifa na biashara vimeongezeka mara tatu katika muongo uliopita na zinaweza kusambaza kwa urahidi wadudu na magonjwa kote dunia na kusababisha uharibifu mkubwa kwa mimea ya asili na mazingitra.

UNEP na FAO wanasisitiza kwamba kulinda mimea dhidi ya wadudu na magonjwa ni saisi zaidi ya kukabiliana na dharura kubwa ya afya ya mimea na kutaka kila mtu, kila nchi na wadau wote kuchukua hatua kuhakikisha afya ya mimea inalindwa.