Skip to main content

Hatimaye mtoto aliyetekwa baada ya mama yake kuuawa Sudan Kusini amerejeshwa:IOM

Baba na mtoto wake baada ya kukutanishwa Juba, wiki tisa baada ya kutoweka katika kisa ambacho alifariki mama yake Isebi, Sudan Kusini.
IOM Photo/Liatile Putsoa
Baba na mtoto wake baada ya kukutanishwa Juba, wiki tisa baada ya kutoweka katika kisa ambacho alifariki mama yake Isebi, Sudan Kusini.

Hatimaye mtoto aliyetekwa baada ya mama yake kuuawa Sudan Kusini amerejeshwa:IOM

Amani na Usalama

Mtoto wa miaka 4 ambaye alitekwa wakati mapigano yalipozuka baina ya makundi yenye silaha mjini Iseb Sudan Kusini Oktoba 27 mwaka 2019 ameachiliwa huru na leo ameunganishwa na baba yake mzani mjini Juba.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM , mtoto huyo ambaye jina lake limehifadhiwa ili kumlinda , ni mtoto wa kiume wa aliyekuwa mfanyakazi wa kujitolea wa IOM ambaye pamoja na mfanyakazi mwezie wa kiume waliuawa baada ya kujikuta katikati ya mapigano hayo walikokuwa wakitoa msaada .

Mwanamke mwingine mfanyakazi wa tatu wa IOM aliyetekwa pamoja na mtoto huyo alifariki dunia kutokana na majeraha aliyopata amesema msemaji wa shirika hilo Jean-Philippe Chauzy na kuongeza kwamba “Tunashukuru sana kwamba mtoto huyu yuko salama na zahma yote ambayo imekuwa ikiendelea kwa takriban wiki kumi ya kumuokoa hatimaye imekwisha. Mvula huyo ameunganishwa tena na baba yake mzazi na sasa tunachojikita nacho ni kuhakikisha wote wanapatiwa ushauri nasaha.”

IOM imeishukuru kamati ya kimataifa ya chama cha msalaba mwekundu kwa msaada na jukumu lake katika kuwezesha kurejea salama mtoto huyo na pia shirika la Umoja wa Mataifa ambalo linatoa msaada wa ushauri nasaha kwa mtoto na baba yake.

Mama wa mtoto huyo alikuwa akifanya kazi katika kituo cha IOM cha uchunguzi wa Ebola kwenye mpaka wa Morobo. Jean-Philippe Chauzy ameongeza kuwa “Wakati tukisherehekea kurejea salama kwa mvulana huyu mioyo yetu imejawa na simanzi kwani tumepokea taarifa kwamba mfanyakazi wetu aliyekuwa amechukuliwa pamoja na mtoto huyo amefariki dunia”.

Kufuatia tukio hilo la mwezi Oktoba mwaka jana IOM ilisitisha kwa muda huduma ya uchunguzi wa Ebola katika maeneo matano ambayo ni Isebi, Bazi, Kirikwa, Lasu na Okaba.

Operesheni katika maeneo mawili ya Bazi na Okaba ilirejeshwa were tarehe 18 Novemba 2019 wakati vituo vingine vitatu bado vimefungwa kutokana na changamoto za usalama zinazoendelea hususan karibu na Lasu.