Sudan Kusini mauaji ya wahudumu wa misaada asilani hayakubaliki:IOM

30 Oktoba 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM leo limelaani vikali mauaji ya wahudumu watatu wa misaada ya kibinadamu wa shirika hilo yaliyofanyika Jumapili kwenye jimbo la Equatoria ya Kati nchini Sudan kusini.

Kwa mujibu wa taarifa ya IOM mauaji hayo ya mwishoni mwa wiki iliyopita yametokea wakati wa mapigano baina ya makundi mawili yenye silaha katika kaunti ya Morobo jimboni Equatoria.

Akizungumzia mauaji hayo ya kusikitisha Jean-Philippe Chauzy mkuu wa IOM nchini Sudan kusini amesema, “tumeshitushwa sana na kuondokewa na wafanyakazi wenzetu na tunatuma salamu za rambirambi kwa familia zao na marafiki. Tunatoa wito kwa wahusika wote wa mauaji hayo ya kikatili dhidi ya raia wasio na hatia na wahudumu wa kibinadamu kufikisha mbele ya mkono wa sheria.”

Wafanyakazi hao wa kujitolea wa IOM mmoja mwanamke na mmoja mwanaume walijikuta katikati ya mapigano yaliyozuka asubuhi ya Oktoba 27 katika kitongoji cha Isebi kaunti ya Morobo. Wanaume wengine wawili wafanyakazi wa kujitolewa wamejeruhiwa katika tukio hilo  na mmoja wao sasa anapatiwa matibabu kutokana na majeraha ya risasi.

Pia katika tukio hilo IOM inasema mwanamke mwingine mfanyakazi wa kujitolea na mtoto mdogo wa miaka minne ambaye mama yake ni mmoja wa wahudumu waliouawa walitekwa katika shambulio hilo na mpaka sasa haijulikani walipo.

Mauti hayo yalipowafika wafanyakazi hao wa kujitolea wa IOM walikuwa wakifanyakazi katika kituo cha upimaji Ebola kwenye maeneo ya mpakani baina ya Sudan kusini, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wakifuatilia kusambaa kwa ugonjwa huo hatari.

Mkurugenzi mkuu wa IOM António Vitorino ameelezea uchungu wake na majonzi kwa mashambulizi dhidi ya raia, “tunaomboleza pamoja na wafanyakazi wetu nchini Sudan Kusini , kwa ajili ya familia za waliopoteza maisha na kurejea kusema kwamba wahudumu wa misaada ya kibinadamu na raia sio walengwa na hawastahili kuwa wahanga wa vitendo hivi vya kikatili na ghasia, sisi sio walengwa.”

Kufuatia tukio hilo IOM imesitisha kwa muda zoezi la upimaji wa Ebola katika vituo vitano vya mpakani vya Isebi, Bazi, Kirikwa, Las una Okaba ikiwemo operesheni za ufuatiliaji na msaada kwa vituo vya afya. Mkuu wa IOM Sudan Kusini Chauzy anafafanua kuhusu uamuazi huo akisema,”usalama wa wafanyakazi wetu ni muhimu sana na hatuwezi kuyaweka zaidi hatarini maisha yao mpaka tuwe na hakikisho la usalama kwa wafanyakazi wetu wote wanaoendesha kazi zao kaunti ya Moboro. Juhudi zetu zinaelekezwa katika kuzisaidia familia zinazoomboleza na narejea kusisitiza ahadi yetu ya kuendelea kuwasaidia watu wa Sudan kusini.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter