Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwaenzi wauguzi na wakunga 2020- WHO Dkt. Tedros

Mwanamke na mtoto wake katika hospitali ya Makara, Cambodia, wakati Nesi akipitia nyaraka zao
World Bank/Chhor Sokunthea
Mwanamke na mtoto wake katika hospitali ya Makara, Cambodia, wakati Nesi akipitia nyaraka zao

Tuwaenzi wauguzi na wakunga 2020- WHO Dkt. Tedros

Afya

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la afya duniani, WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, kupitia salamu zake za mwaka mpya wa 2020 ametoa wito wa kuwaenzi kwa kila namna wahudumu wa afya hususani nesi na wakunga.

Ili kusisitiza umuhimu wahudumu wa afya, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus anaaza salamu zake kwa kuwashukuru watoa huduma za kiafya kote duniani.

Anasema wanafanya kazi hata katika nyakati za mapumziko ambazo wengine wanakuwa majumbani na wapendwa wao.

Tedros anasema lakini dunia inapaswa kufanya vizuri zaidi kuwasaidia wahudumu wa afya, kuwalipa vizuri, kuwapa mafunzo na kuwalinda.

“Kwa miaka 10 tunakadiria dunia itahitaji wahudumu wa afya wengine milioni 18, zaidi katika nchi za kipato cha chini na cha kati,” anasema Skt Ghebreyesus.

Anasisitiza akisema Mwaka 2020 ni mwaka wa Nesi na Wakunga

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva
Picha ya UN/Elma Okic
Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva

Katika mwaka huu, WHO na wadau wake watazisihi nchi kuboresha elimu na ajira kwa nesi na wakunga.

Dkt Ghebreyesus anasema ni wa muhimu kutokana na ukubwa wa huduma za kiafya wanazozitoa, kuanzia hatua za kwanza za maisha hadi mwisho.

“Asilimia 70 ya wafanyakazi wa afya duniani ni wanawake, kwa hivyo kazi kwa wafanyakazi wa afya mara nyingi ni za wanawake.” Anafafanua Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

Anaongeza kwa kusema, kuwekeza katika wafanyakazi wa afya kunalipa mara tatu katika afya, ukuaji wa uchumi na usawa wa kijinsia.

“Na kwa hivyo, mwaka mmoja unapoisha na mwingine unapoanza, nataka kutoa shukrani zangu za dhati kwa wafanyikazi wa afya kila mahali.” Anashukuru Dkt Ghebreyesus akimalizia kwa kusema anazifikiria familia hasa za wale waliopoteza maisha yao wakiwa katika harakati za kuokoa maisha yaw engine katika mwaka uliopita wa 2019, na hapo anamtaja Dkt Richard Mouzoko na Belinda Kasongo.