Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya haki za binadamu Libya ni mbaya-OHCHR

Taswira kupitia dirisha la chuma ikionyesha mazingira ya wahamiaji waliolala kwenye magodoro sakafuni kwenye moja ya vituo vya kushikilia wahamiaji nchini Libya
UNICEF/Romenz
Taswira kupitia dirisha la chuma ikionyesha mazingira ya wahamiaji waliolala kwenye magodoro sakafuni kwenye moja ya vituo vya kushikilia wahamiaji nchini Libya

Hali ya haki za binadamu Libya ni mbaya-OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, imeeleza wasiwasi ilionao kuhusu kuzorota kwa hali ya haki za binadamu nchini Libya.

Kupitia taarifa iliyotolewa hii leo na Rupert Colville ambaye ni msemaji wa ofisi hiyo mjini Geneva Uswisi, OHCHR imesema kudorora kwa hali ya haki za binadamu ni pamoja na mgogoro unaoendelea kati ya raia, mashambulizi dhidi ya watetezi wa haki za binadamu na wanahabari, wanavyotendewa wahamiaji na wakimbizi, na hali katika kambi zinazowashikilia wahamiaji.

Bwana Colville amesema,“katika mwaka 2019, ofisi yetu pamoja na UNSMIL hadi sasa wameorodhesha vifo vya raaia 284 na majeruhi 363 kwa sababu ya vita vya kijeshi nchini Libya-Ongezeko la zaidi ya robo ya idadi ya majeruhi waliowekwa katika kumbukumbu katika kipindi kama hicho cha mwaka uliopita.”

Akiendelea kueleza hali ilivyo nchini Libya, msemaji huyo wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema, mashambulizi ya anga yalikuwa sababu kubwa ya vifo vya raia ikiwemo vifo 182 na majeruhi 212, yakifuatiwa na mapigano ya ardhini, vilipuzi vya kutegwa ardhini ambavyo vilikuwa vimesalia bila kulipuliwa, utekaji na mauaji.

Katika kipindi kama hicho, Shirika la Afya duniani, WHO, waliandika mashambulizi 61 yanayohusiana na mgogoro yakilenga vituo na wahudumu wa afya, ambayo ni obgezeko la asilimia 69 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

"Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu athari za mzozo katika maeneo yenye watu wengi kama Abu Salim na Al Hadba, ambapo raia 100,000 zaidi wako hatarini kufurushwa katika makazi yao, watu 343,000 tayari wameshafurusha.” Amesema Bwana Colville.

Taarifa ya OHCHR, imeeleza kuwa wanahabari, wafanyakazi wa vyombo vya habari na wanaharakati wa haki za binadamu wanaendelea kulengwa na vurugu, vitisho na manyanyaso. Katika kisa cha hivi karibuni, Reda Fhelboom, mwanahabari na mpigania haki za binadamu, alishikiliwa kizuizini tangu Desemba 14 na kundi lenye silaha katika Uwanja wa ndege wa Mitiga mjini Tripoli alipotua akitokea Tunis Tunisia.

Aidha suala la wanavotendewa wahamiaji na wakimbizi limeibua wasiwasi mkubwa kutokana na matendo mabaya wanayotendewa ikiwemo kukamatwa pasipo kufuata sheria, mauaji, mateso na unyanyasaji kingono, utekwaji, kutumikishwa na usafirishaji binadamu kiharamu.