Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya fungulieni vituo vya televisheni mlivyofunga- UN

Maandamano ya kupinga ubinyaji wa uhuru wa vyombo vya habari.
UNESCO/C.Darmouni
Maandamano ya kupinga ubinyaji wa uhuru wa vyombo vya habari.

Kenya fungulieni vituo vya televisheni mlivyofunga- UN

Haki za binadamu

Tuna wasiwasi mkubwa kuwa vituo vitatu vya televisheni nchini Kenya bado vimefungwa kwa siku ya tatu sasa, imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu hii leo. Siraj Kalyango na maelezo zaidi.

Vituo hivyo vitatu vya televisheni ni Citizen, KTN na NTV ambapo yadaiwa vilifungiwa na serikali ya Kenya baada ya kukiuka agizo la kutotangaza kile kilichoitwa ni sherehe ya kumwapisha Raila Odinga aliyejitangaza kuwa Rais wa Kenya.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa ofisi hiyo, Rupert Colville amesema wana hofu pia juu ya majaribio ya serikali ya kuingilia uhuru wa kujieleza kwa kitendo chake cha kuonya kuwa ushiriki wowote wa hafla hiyo ungalisababisha kufutwa kwa leseni na hivyo vyombo vya habari vilivyokiuka ushauri huo vilifungiwa.

(Sauti ya Rupert Colville)

“Tunaelewa kuwa vituo hivi vimeendelea kufungiwa licha ya agizo la mpito lililotolewa na Mahakama ya Kuu ya Kenya la kutaka serikali iruhusu vituo hivyo viendelee na matangazo. Tunatoa wito kwa serikali iheshimu na itekeleze uamuzi huo wa mahakama.”

Tunasihi serikali na upinzani nchini Kenya washirikiane kutatua hali ya sasa kwa njia ya mazungumzo huku wakiheshimu sheria za kimataifa na haki za kujieleza, kisiasa, mikusanyiko na kujiunga na vyama.