Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zimbabwe acheni msako dhidi ya waandamanaji- OHCHR

Rupert Colville, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR
UN Photo.
Rupert Colville, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR

Zimbabwe acheni msako dhidi ya waandamanaji- OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR , imeisihi serikali ya Zimbabwe isake njia bora ya kushughulikia machungu ya hali ngumu ya kiuchumi inayokumba wananchi badala ya kushambulia waandamanaji wanaolalama kuhusu mazingira duni.

 

Msemaji wa ofisi hiyo Rupert Colville amesema hayo leo mjini Geneva, Uswisi wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya ripoti ya kwamba maandamano yaliyokuwa yamepangwa leo yamefutwa muda mfupi tu kufuatia Mahakama Kuu kukazia msimamo wa serikali wa kupiga marufuku maandamano hayo.

Inaelezwa kuwa tayari waandamanaji walikuwa wamekusanyika na baada ya tangazo hilo la mahakama, walisambaratishwa na polisi huku ikiripotiwa kuwepo kwa matumizi ya nguvu dhidi ya watu hao.

“Huku kukiwa na uwezekano wa maandamano kufanyika tena Zimbabwe katika siku zijazo, tunasihi serikali isake njia sahihi na za kisheria za kujadiliana na wananchi kuhusu machungu yao. Iwapo maandamano yanaendelea tunasihi vikosi vya usalama na waandamanaji wahakikishe kuwa yanafanyika bila ghasia,” amesema Bwana Colville.

Ameelezea wasiwasi wake kuhusu janga la kijamii linaloendelea kuibuka nchini Zimbabwe akisema kuwa, “wakati tunatambua juhuduiza serikali, jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa nchini Zimbabwe za kupunguza machungu ya madhara ya kijamii na mchakato wa marekebisho, hali ngumu ya kiuchumi inakwamisha wananchi kupata haki yao ya kiuchumi na kijamii.”

Bwana Colville amesema kipindi kirefu ya kutochukua hatua na udhaifu wa mifumo ya utendaji vimesababisha mfumuko wa bei uliochochea ongezeko la bei za mafuta, vyakula usafiri na huduma za afya, “hali ambayo imekuwa na madhara makubwa kwa wananchi hususan wafanyakazi wa pembezoni.”

Amegusia pia suala la watu kushambuliwa na kuswekwa rumande kiholela hususan viongozi wa mashirika ya kiraia.

Msemaji huyo wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa mamlaka za serikali zina wajibu wa kuhakikisha watu wanatekeleza haki yao ya kujieleza sambamba na kukusanyika kwa amani.
“Tunasihi Baraza la Seneti wakati linapitia muswada wa usimamiaji wa amani na utulivu lihakikishe kuwa haki za msingi za uhuru wa kujieleza na kuandamana zinazingatia katiba na uamuzi wa Mahakama ya Katiba na sheria za kimataifa za haki za binadamu,” amesema Bwana Colville. 

Halikadhalika amesihi serikali ya Zimbabwe iongeze jitihada zake marudufu za kushughulikia changamoto za sasa kupitia mazungumzo ya kitaifa.