Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado haki za mtoto zinasiginwa- Bachelet

Pichani ni Kiara mtoto mwenye umri wa miaka 5 akiuza vibanio vya nywele ndani ya  treni. Kiara amekuwa akifanya biashara hii tangu akiwa na umri wa miaka mitatu.
UNICEF/UNI103753/Rich
Pichani ni Kiara mtoto mwenye umri wa miaka 5 akiuza vibanio vya nywele ndani ya treni. Kiara amekuwa akifanya biashara hii tangu akiwa na umri wa miaka mitatu.

Bado haki za mtoto zinasiginwa- Bachelet

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC duniani, bado haki hizo za msingi zinaendelea kusiginwa.

Bi. Bachelet amesema hayo hii leo huko Geneva, Uswisi wakati akifungua mkutano wa 80 wa kamati ya mkataba huo wa haki za mtoto wakati huu ambapo unatimiza miaka 30 tangu kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mkataba huo unataja haki kuu nne za msingi za mtoto ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kushirikishwa na kulindwa, ambapo Bi. Bachelet amesema..

“Takribani kila nchi mwanachama wa mkataba imepitisha sheria za kulinda haki za mtoto na kuweka mipango ya kusongesha haki hizo ambazo si tu zinamnufaisha mtoto bali pia jamii nzima. Mipango ya elimu, lishe, huduma za afya imekuwa na manufaa makubwa duniani kote.”

Hata hivyo amesema bado watoto wanakabiliwa na madhila.

 

Mathalani amesema mwaka 2012 pekee, zaidi ya watoto milioni 5.5 walikuwa manusura wa utumikishwaji kazini, mamilioni ya watoto wa kike waliozwa mapema na kupata watoto wangali watoto, na ni vigumu kupata takwimu halisi ya watoto waliotumikishwa na vikundi vilivyojihami kwenye mizozo.

Kamishna Mkuu huyo wa haki za  binadamu amesema katika mazingira kama hayo, ndoto na matarajio ya watoto hao vinatumbukia nyongo, kwa hiyo amesema..

“Maadhimisho ya mwaka huu ya miaka 30 ya CRC ni fursa muhimu ya kuchechemua umuhimu wa misingi ya mkataba huo na malengo yake. Nafurahi kuungana na UNICEF kuitisha mjadala wa wazi wakati wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba na mkutano mwingine mwezi Novemba ambao utatumia teknolojia kuunganisha matukio yote ya kimataifa duniani kote.”